Korea Kaskazini yapeleka wanajeshi Urusi

KOREA KASKAZINI : SERIKALI ya Korea Kaskazini imetuma wanajeshi wengine kuisaidia Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la serikali, KCNA, wanajeshi wa taifa hilo walishiriki katika operesheni za kukomboa eneo la mpaka wa Kursk, kufuatana na amri ya kiongozi wao Kim Jong Un.
Hatua hiyo inakuja baada ya Mkuu wa Majeshi wa Urusi, Valery Gerasimov, kusifu ushujaa wa wanajeshi wa Korea Kaskazini, hatua iliyothibitisha kwa mara ya kwanza kushirikiana kwa majeshi hayo katika vita.
KCNA ilieleza kuwa uamuzi wa kupeleka wanajeshi umetokana na mkataba wa ulinzi wa pande mbili uliotiwa saini kati ya Pyongyang na Moscow.
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, alinukuliwa akiwapongeza wanajeshi wake kwa “kuwakilisha heshima ya taifa,” huku akisisitiza kuwa damu iliyomwagika Kursk imedhihirisha muungano wa undugu kati ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo, Ukraine imekanusha madai kuwa Urusi imedhibiti kikamilifu eneo la Kursk, huku idara za ujasusi za Korea Kusini na mataifa ya Magharibi zikiripoti kuwa Pyongyang ilituma wanajeshi maelfu mwaka jana. SOMA: G7 wailaumu Korea Kaskazini kutuma wanajeshi Urusi
Ripoti kuhusu wanajeshi wa Korea Kaskazini kutumwa zilianza kuibuka mwezi Oktoba, kufuatia kuimarika kwa uhusiano kati ya Kim Jong Un na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Taarifa zinaeleza kuwa makubaliano ya usaidizi wa kijeshi yalitiwa saini, huku taarifa nyingine zikidai kuwa maelfu ya wanajeshi wa Korea Kaskazini walihusika kwenye mapigano na takriban watu 1,000 kati yao waliuawa ndani ya kipindi cha miezi mitatu.