Korea Kusini yavutiwa mkakati nishati safi

KOREA Kusini imesema iko tayari kuunga mkono jitihada za kutekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia ulioasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Ahn Eunju amesema serikali ya nchi hiyo imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao ni muhimu kwa maendeleo ya ustawi wa jamii.
Amesema hayo alipokutana na kuzungumza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kando ya Mkutano wa Mafuta na Gesi kwa nchi za Afrika Mashariki unaoendelea Dar es Salaam.
“Serikali yetu inaunga mkono ajenda hii ya nishati safi inayobebwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambayo ni muhimu sana kuendelea kutekelezwa kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Nishati,” amesema.
Dk Biteko alisema Tanzania imepiga hatua katika kuwezesha wananchi kupata unafuu wa maisha kwa kupata na kutumia nishati safi na hivyo kuepukana na madhara yanayotokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi yakiwemo magonjwa na vifo.
Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia wa miaka 10 unakusudia kuwawezesha asilimia 80 ya Watanzania kuwa watumiaji wa nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Tunaendelea kutekeleza mkakati huu kwa kubadilisha mtazamo wa watu waliokuwa wakitumia vyanzo vya asili vya
nishati ambavyo sio salama, lakini tunaendelea kubadili mitazamo yao ili waweze kuungana na jitihada hizi za kitaifa na kimataifa za matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Dk Biteko.
Amesema kuna jitihada kimataifa ikiwa ni pamoja na kusainiwa makubaliano kuhusu matumizi ya nishati kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu.
Aidha, alisema ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi hauepukiki ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi Barani Afrika tulisaini makubaliano kadhaa ikiwa ni pamoja na kupata fedha ili kuwawezesha wahitaji kuboresha maisha yao kupitia Nishati Safi,” amesema Dk Biteko.