Kriketi wanawake watinga nusu fainali Kwibuka

TIMU ya taifa ya wanawake ya kriketi ya Tanzania imetinga nusu fainali katika mashindano ya Kwibuka nchini Rwanda kwa ushindi wa kishindo wa mikimbio 119 dhidi ya Cameroon katika mchezo wa mwisho hatua ya ligi uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Gahanga, Kigali.

Tanzania imefuzu hatua hiyo ikiwa miongoni mwa timu nne bora baada ya kumaliza mechi za Ligi katika nafasi ya tatu kati ya timu tisa shiriki. Wenyeji Rwanda iliongoza msimamo ikifuatiwa na Uganda, huku Zimbabwe ikichukua nafasi ya nne.

Katika mchezo huo dhidi ya Cameroon, Tanzania ilianza kwa kupiga kwanza na kufikisha jumla ya mikwaju 172 kwa wachezaji watatu (172/3) ndani ya overs 20.

Nahodha wa Tanzania, Fatuma Kibasu, aliongoza mashambulizi kwa kufikisha mikwaju 59 kwa mipira 56, akiweka msingi imara kwa ushindi wa timu yake.

Kwa upande wa Cameroon, walijikuta wakilemewa na mashambulizi ya Tanzania na kufungwa wote kwa mikwaju 53 ndani ya overs 18.2. Mchezaji aliyefanya jitihada zaidi kwa Cameroon alikuwa Madaleine Sissako, aliyefunga mikwaju 11 kwa mipira 31.

Tanzania ilionesha ubora katika upande wa kupiga na kuzuia (bowling), ambapo Tabu Omary aliibuka na mafanikio makubwa kwa kuchukua wiketi 4 kwa mikwaju 13 ndani ya overs 4, akiweka rekodi bora ya mchezo huo.

Kwa upande wa Cameroon, Clemence Manidom alipata mafanikio madogo kwa kupata wiketi moja kwa mikwaju 15 katika over moja tu aliyocheza.

Mchezaji Bora wa mechi alitangazwa kuwa Fatuma Kibasu kutokana na mchango wake mkubwa katika ushindi huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button