Krismasi kuadhimishwa kitaifa Kigoma
IBADA ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi inafanyika kitaifa leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kanisa Kuu la Kigoma.
Kwa upande wa ibada ya Krismasi kitaifa, itafanyika kesho katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Bikira Maria Mshindaji, Jimbo Katoliki la Kigoma.
Kaimu Ofisa Habari na Mawasiliano wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), David Madinilo alisema ibada ya mkesha leo itaendeshwa na CCT na kuongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Magharibi, Jackson Mushendwa.
SOMA: Krismasi, Mwaka Mpya 2026 ziwe msingi wa amani
Kuhusu ibada ya Krismasi, taarifa ya awali ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) iliyosainiwa na Padri Furaha, imeeleza kwamba misa takatifu itaanza saa 2:30 asubuhi katika kanisa hilo la kiaskofu mjini Kigoma.
Maadhimisho yataongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Joseph Mlola yakiwa na ujumbe mkuu wa matumaini.
Desemba 25 Wakristo nchini huungana na wenzao duniani kuadhimisha kumbukizi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, takribani miaka 2,000 iliyopita.
Kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na Mwaka Mpya, Jeshi la Polisi limesema litaendelea kuimarisha ulinzi wakati wote, kabla na baada ya sikukuu hizo ili Watanzania washerehekee kwa amani.
Katika taarifa yake ya juzi, Jeshi la Polisi lilitoa wito kwa wananchi kutambua thamani na umuhimu wa amani na usalama katika maisha ya kila mmoja.
Wakati huo huo, jeshi hilo limetoa wito kwa wasafiri kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, wakizingatia kaulimbiu ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani: “Endesha Salama, Familia Inakusubiri.”


