SERIKALI imesema kuanzia Januari mwakani somo la biashara litaanza kufundishwa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema somo hilo litakuwa ni la lazima kwa wanafunzi wote.
Profesa Mkenda alisema hayo Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa jukwaa la wadau wa sekta ya fedha.
Alisema wizara hiyo imetambua umuhimu wa masuala ya uchumi na fedha na imeandaa mtaala mpya wa elimu utakaowawezesha wanafunzi kupata elimu ya ujasiriamali na biashara ili kuwajengea maarifa ya kujikwamua kiuchumi.
“Kuanzia mwezi wa kwanza watu wanaingia kidato cha kwanza ni lazima kila mwanafunzi asome somo la biashara lakini hasa ujasiriamali,” alisema.
Profesa Mkenda alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuwaanda vijana wanaomaliza kidato cha nne waweze kujitegemea na mhitimu akiamua kuingia kwenye shughuli zake mwenyewe ajue anajipanga vipi.
“Tunataka kijana akimaliza kidato cha nne anajua Brela ni nini, akitaka kwenda benki anafanyaje,Tin namba ni nini, TRA kazi yake ni nini, muhimu zaidi kuwekaje kumbukumbu zako,” alisema.
Profesa Mkenda alisema sekta ya elimu ina mchango mkubwa kuboresha sekta ya fedha, hivyo mkutano huo ni muhimu ili kupata maoni ya sekta ya fedha katika kuboresha mtaala huo.
“Tunahitaji kutengeneza wataalamu ambao watatusaidia kusukuma gurudumu letu kwenda mbele, changamoto ya mitaji kuunganisha wenye fedha na wanaohitaji mitaji ni kazi moja muhimu sana,” alisema.