Kuhifadhi mbegu za uzazi Sh milioni moja

DAR ES SALAAM – KITUO cha kupandikiza mimba cha Dk Samia Suluhu Hassan katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kimesema mtu anayehitaji kupata mtoto anaweza kuhifadhi mbegu za uzazi kwa gharama ya Sh milioni moja kwa mwaka.

Mkuu wa Kitengo cha Upandikizaji Mimba katika kituo hicho, Dk Matilda Ngarina ameshauri wenye kuhitaji kuhifadhi mbegu za uzazi wahifadhi muungano wa mayai ya kike na mbegu za kiume.

Dk Ngarina alisema ikiwa mtu ameamua kuhifadhi mbegu kwa muda mrefu ni vizuri ahifadhi mchanganyiko huo kuepuka kupungua ubora kadri muda unavyozidi kwenda kutokana na baridi iliyopo katika sehemu ya kuhifadhia.

Advertisement

“Tunahifadhi kutokana na mahitaji na kama kuna wagonjwa ambao labda wanaenda kwenye matibabu ya saratani, hao unaweza kuwahifadhia japokuwa hatushauri sana mbegu za kike tu au za kiume tu,” alisema.

Aliongeza, “…ni vizuri mtu kuhifadhi embryo ambayo ni muunganiko wa mbegu ya kike na ya kiume, hizo ndizo zinakaa muda mrefu lakini mbegu ya aina moja tu ya kike tu au ya kiume tu muda unavyozidi kwenda huwa ubora nao unazidi kupungua”.

SOMA: Rais Samia kubariki Kongamano la Afya 

Dk Ngarina alisema ikiwa mwanamke atahitaji kuchangiwa mbegu za kiume na akampata mchangiaji, gharama ya mbegu hizo za kiume watakubaliana wenyewe.

Alisema kama mchangiaji atatafutwa na kituo watamsikiliza mchangiaji na kwamba gharama ya kuhifadhi mbegu hizo zitalipwa na aliyehitaji huduma.

“Kwa sababu ndio kwanza tunaanza, tunataka mtu ambaye anataka mtoto ikiwa hawezi kutoa mbegu yeye mwenyewe alete mtu wakubaliane sisi tutamhifadhia mbegu zake,” alisema Dk Ngarina.

Alisema mchangiaji na anayechangiwa mbegu ndio watakubaliana kama watahitaji mchangiaji atambulike kama baba wa mtoto atakayezaliwa au la.

Dk Ngarina alisema umeandaliwa muswada wa sheria ya kuongoza huduma za kupandikiza mimba na lakini kwa sasa zipo fomu za makubaliano ambazo mchangiwaji atatakiwa kusaini kabla ya kufanyiwa upandikizaji. Alisema nyaraka hizo zinakuwa za kisheria na kama makubaliano yatakiukwa, fomu hizo zinakuwa rejea. Kituo hicho ni cha kwanza kutoa huduma hiyo kwa upande wa hospitali za umma nchini.

MNH inapandikiza mimba kwa Sh 14,000,000. Dk Ngarina alisema kati ya wanawake 10 waliokuwa tayari kwa ajili ya huduma ni wanne walikuwa wamelipa na akasema upandikizaji huo hufanyika kwa makundi hivyo litahitajika kundi la watu kuanzia watano hadi 10.

Septemba 12 mwaka huu, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alizindua kituo hicho cha kupandikiza mimba MNH. Serikali pia imesisitiza upimaji afya utafanyika nyumba hadi nyumba