Rais Samia kubariki Kongamano la Afya

DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la 11 la Afya Oktoba Mosi katika Mji wa Fumba, Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya imesema kuwa kongamano hilo la kihistoria, linalenga kuwapa fursa wadau na wataalamu wa afya kukutana ili kubuni njia za pamoja katika kuboresha sekta ya afya nchini Tanzania.

 

Advertisement

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

“Ni matarajio yetu, fursa hii itatupeleka mbele katika dhamira yetu ya kuboresha huduma za afya kwa wote,” imeeleza taarifa hiyo.

Moja ya tukio muhimu katika kongamano hilo ni Mkutano wa Oktoba 03 katika Ukumbi wa Spice, ZITF, kisiwani Unguja, Zanzibar ambapo watekelezaji wa mradi wa Afya-Tek, Apotheker, D-tree na wengine watamulika jinsi teknolojia inavyoboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wote, kujenga daraja kati ya sekta binafsi na sekta ya umma ili kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa viwango vya juu na kwa uendelevu.

Mojawapo ya mijadala muhimu katika kongamano hili ni kuangazia namna mpango wa Afya-Tek, unaotekelezwa na Apotheker, D-tree, na washirika wake, unavyolenga kutoa huduma bora kwa kuunganisha sekta binafsi kupitia maduka ya dawa muhimu yaliyoidhinishwa (DLDM) na Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii (WAJA) pamoja na Vituo vya Afya .

Mpango huu unalenga kuanzisha mfumo endelevu wa huduma za afya ambao unasaidia kusanifisha huduma kati ya sekta za umma na binafsi, pia watoa mada watazungumzia mafanikio na changamoto za ubunifu wa kidijitali katika sekta ya afya.

Kongamano hilo litafungwa na mwenyeji wa visiwani, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi mnamo Oktoba 03.

SOMA: Serikali: Bima ya Afya kwa wote itarahisisha huduma

SOMA: Watu 1,000 kufikiwa afya bure Ifakara