Watu 1,000 kufikiwa afya bure Ifakara
IFAKARA, Morogoro: MENEJA wa Mfuko wa Bima ya Afya nchini (NHIF) Mkoa wa Morogoro, Mbala Shitindi amesema wanatarajia kuwafikia takribani watu 1,000 katika programu ya siku tano ya uhamasihaji, usajili na upimaji wa afya bure.
Ameyasema hayo leo Agosti 26 ndani ya Soko Kuu la Halmashauri ya Mji wa Ifakara wakatu akifungua programu hiyo inayojumuisha upimaji bure wa magonjwa ya presha, sukari pia uchunguzi wa Uwiano wa Urefu na Ufupi (BMI).
“Zoezi hili la uhamasishaji ni utangulizi kuelekea utekelezaji wa sheria mpya ya Bima ya Afya kwa wote iliyosainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Shitindi.
Shitindi amesema lengo la programu hiyo ni kuhakikisha wananchi wana uelewa juu ya umuhimu wa kujiunga na bima ya afya, namna ya kujiunga na namna inavyofanya kazi.
“Kwa mchango wa kuanzia ni kiasi cha Sh. 192,000 utapata kadi itakayokupa fursa ya kutibiwa popote nchini katika vituo zaidi ya 9,000 vya Tanzania Bara na Visiwani ambayo ni zaidi ya asilimia 90 ya vituo vya afya na hospitali zilizopo nchini,
“Ukiwa na kadi ya Bima ya Afya ni sawa na kutembea na daktari na dawa mfukoni mwako,” amesema meneja huyo.
SOMA: Mpango Bima ya Afya kunufaisha wasanii
Yusufu Majalali, Mkazi Ifakara ameambatana na mkewe, Halima Kondo ambao ni wanufaika wa program hiyo leo Agosti 26 wameeleza kufurahishwa na huduma waliyopata katika Soko Kuu la Ifakara, ambapo inafanyika programu ya NHIF.
“Nimepimwa vizuri na baada ya kupimwa kweli nimekutwa na sukari 22 ‘ugonjwa wa sukari’ na shinikizo la damu (BP) 200,” ameeleza Kondo.
SOMA: Elimu wataalamu wa afya ni uwekezaji-Prof Msofe
Amesema wameshauriana na mume wake kufika hospitali ya Mtakatifu Francis iliyopo Ifakara ili kuanza kliniki ya sukari.
“Kwakweli mimi na mke wangu tumeshauriana na kuamua ni vyema kujiunga na NHIF kwani inafaida kubwa kwetu pia sisi binadamu tunatembea na ugonjwa, hatujui lini tutazidiwa,” amenukuliwa Majalali.