Mpango Bima ya Afya kunufaisha wasanii
WASANII nchini huenda wakanufaika na mpango wa huduma ya Bima za Afya na bima ya maisha kwa wasanii wote nchini. Mpango huo unaendelea kujadiliwa baina ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Kampuni ya Galco Insurance.
Taarifa iliyotufikia dawati la habari ni kuwa viongozi wa BASATA na kampuni hiyo wamekutana leo kufanya kikao kujadili kuhusiana na mpango huo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa, Dk Kedmon Mapana ameongoza kikao hicho na wajumbe wa Basata pamoja na ugeni kutoka kampuni hiyo iliyo chini ya GSM.
“Tumepokea ugeni uliongozwa na Emmanuel Bugangu ambaye ni meneja wa kampuni ya bima ya GALCO Insuarance Brokers akiwa na Ian Mmbando ambaye ni meneja uendeshaji wa kampuni hiyo ambapo lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutengeneza mpango wa ushirikiano wa utoaji wa Bima za Afya na bima ya maisha kwa wasanii nchini,”amesema Dk Mapana.
SOMA: BASATA latoa siku saba wasanii kujisajili
Dk Mapana amewapongeza GALCO Insurance Brokers kwa kuwa na mpango wa uwezeshaji mzuri wa upatikanaji wa huduma za bima kwa wasanii na kongeza kuwa Baraza la Sanaa la Taifa lipo tayari kushirikiana nao ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hiyo kwa Wasanii nchini.
Aidha, Meneja wa kampuni hiyo, Emmanuel Bugangu amesema kuwa lengo la mpango wa utoaji wa bima hizo kwa wasanii na wadau wa sanaa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wasanii na wadau wote wa sanaa.