‘Kujituma, ubunifu vitaondoa changamoto za kiuchumi’

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene amesema changamoto nyingi za kiuchumi katika jamii zitatauliwa endapo wananchi watajituma kufanya kazi na kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali kama ambavyo maandiko matakatifu yanaagiza watu kufanya kazi.

Alisema hayo hivi karibuni wakati wa sherehe ya kumweka wakfu Askofu wa tatu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto iliyofanyika Jijini Dodoma baada ya aliyekuwa askofu wa kanisa hilo, Donald Mtetemela kumaliza muda wake.

Aliwataka Wakristo kote nchini kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo na kuchangia pato la taifa na kutatua changamoto zilizo katika maeneo yao.

Alisema kuwa serikalii itaendelea kushirikiana na taasisi za dini kwani zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, kusimamia maadili na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watu wasio na hofu ya Mungu.

“Licha ya mchango mkubwa wa kanisa hili kwa serikali lakini kumekuwa na mmomonyoko wa maadili, magonjwa na majanga, hivyo ni muhimu kushirikiana na serikali ili kuokoa vijana na watoto wetu. Matumaini yetu ni kwamba viongozi wa dini mkiendelea kusimama imara na kutoa huduma ya kiroho tutatatua changamoto hii,” alisema.

Aidha alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ufisadi, utovu wa nidhamu kwa watumishi wa umma pamoja na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Mhashamu Dk Mahimbo Mndolwa aliipongeza serikali kwa kuwa mstari wa mbele kuziunga mkono taasisi za dini katika nyanja zote huku akimtaka Askofu Chiteto kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu na kufikia malengo ya kanisa yaliyowekwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button