Kuporomoka jengo K’Koo: Mmoja afa, 28 waokolewa

Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wameungana na vikosi vya uokoaji kuimarisha juhudi hizo.

DAR ES SALAAM – Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mwili mmoja na majeruhi 28 wameopolewa kutoka kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, mapema leo. 

Jitihada za uokoaji zinaendelea huku juhudi zikielekezwa kuwaokoa waliobaki chini ya kifusi hicho.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo la ajali, Majaliwa amewataka wananchi na wafanyabiashara kuwa watulivu na kuruhusu mamlaka husika kufanya kazi yao.

Advertisement

“Mpaka sasa, mwili wa mtu mmoja umeopolewa, na majeruhi 28 wamepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali jirani kwa matibabu,” amesema Waziri Mkuu, bila kuthibitisha idadi kamili ya walioko chini kifusi ama majeruhi waliopelekwa katika hospitali zingine.

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole na kuagiza mamlaka husika kufanya kila linalowezekana kufanikisha uokoaji. 

“Nimeagiza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Zimamoto, na Hospitali ya Muhimbili kuhakikisha jitihada hizi zinafanyika kwa haraka na ufanisi. 

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Tuendelee kuwaombea majeruhi wapone haraka,” alisema Rais Samia ambaye anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi nchini Brazil.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa baadhi ya manusura wamebainisha kuwapo kwa watu wengi zaidi waliofunikwa na kifusi. Mama mmoja ameeleza kuwa bado anawasiliana na mtoto wake aliye chini ya kifusi kupitia simu. Mfanyabiashara mwingine alisema vijana wake wawili walioko chini ya kifusi hawajapatikana, na simu zao hazipatikani.

Jitihada za kuongeza oksijeni kwa walioko chini ya kifusi zinaendelea. Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wameungana na vikosi vya uokoaji kuimarisha juhudi hizo.

Rais Samia ameendelea kusisitiza mshikamano na utulivu wakati mamlaka zikiendelea na shughuli za uokozi. Kwa mujibu wa taarifa rasmi, juhudi hizi zinalenga kuhakikisha kila aliyefunikwa anafikiwa haraka iwezekanavyo.