Kusema ajali haina kinga ni kuendelea kujimaliza
AJALI haina kinga na alipangalo Mola hakuna mja anaweza kulipangua ni baadhi ya semi ambazo zimekuwa zikitumika sana baada ya ajali au maafa kutokea.
Semi hizi zinaweza kuwa ni moja kati ya sababu ambazo zinazopelekea ajali ziendelee kutokea kwa kuwa watu wanaamini kuwa kama Mungu alipanga ajali itokee basi itatokea tu hata kama mlikuwa mnaendesha kwa mwendo wa taratibu kiasi gani.
Wakati mwingine inafaa kuangalia ukweli wa mambo, kuna mambo tunamtwisha Mungu ambayo yanakwenda kinyjme na busara na hekima alizotupa yeye aliyetuumba.
Makamanda wa vikosi vya usalama barabarani wamekuwa wakitoa elimu kwa madereva na wasafiri ambao kuhusu usalama wao lakini mara zote ajali inapotokea tunaambiwa mwendo ulikuwa si wa kawaida.
Mathalani mwishoni mwa wiki ilitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu 5 na wengine 56 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Najimunisa iliyokuwa ikitokea Dar es salaam kuelekea mkoani Mwanza kugongana uso kwa uso na roli katika eneo la Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga.
Katika tukio hilo tumemsikia Kaimu kamanda wa Polisi, Leornad Nyandahu, pamoja na manusura wa ajali hiyo wakisema chombo chao, Najimunisa, kilikuwa kinakaribia ‘kupaa’ yaani mwendokasi ulikuwa na kasi kwelikweli.
Ukweli huu unaouma ndio unaotukuta siku zote baada ya ajali, eti mwendokasi ulikuwa kasi kwelikweli.

Ndio kusema pamoja na jitihada zote za Polisi na wadau wengine kuhakikisha kwamba ajali zinapungua kwa kushawishi madereva na abiria kuzingatia mwendo na usalama barabarani, abiria na madereva wanakubaliana kutokukubaliana kuhusu usalama wao.
Kwa sababu abiria kama wangempigia kelele dereva ajali ile isingetokea na kama ingetokea ingekuwa na maumivu kidogo kuliko sasa.
Basi ni wakati sasa kutilia nguvu mambo ambayo yatasaidia kupunguza ajali na kuanzisha mambo mapya.
Mosi kuendelea kutoa elimu kwa abiria kuhusu usalama na wajibu wao pindi wanapokuwa katika vyombo vya usafiri, watu wengi wanadhani kuwa usalama wa maisha yao upo mikononi mwa askari wa usalama barabarani kitu ambacho sio sawa .
Aidha mamlaka ambazo zinauwezo wa kuwachukulia hatua madereva ambao watakuwa wakiendesha bila kutii sheria na kuhatarisha maisha ya watu zifanyekazi zao ili kuondokana na adha hii.
Pili askari ambao wamepewa dhamana ya kusimamia sheria na mienendo ya magari barabarani kusimamia sheria bila ya kuwa na huruma kwani huruma yao ndio mauti yetu.
Tatu ambao wamepewa jukumu la kutunga sheria za barabarani waangalie upya juu ya sheria zinazoadhibu wakosaji wote ambao wanafanya makosa ya barabarani kwani kulipa faini na kufungia leseni kwa muda fulani inaonekana kuzoeleka. Mtu akifanya kosa anajipanga kulipa faini ambayo mara nyingi huwa sio pesa kubwa ama anakaa kwa muda fulani bila kuendesha.
Pia wasimamizi wa barabara kuhakikisha kuwa matengenezo yanafanyika kwa wakati na ustadi wa hali ya juu na kuweka alama zinazohitajika katika sehemu husika ili kuondoa uwezekano wa kutokea kwa ajali.
Mwisho niwashauri madereva na wasio madereva kuwa usemi wa ajali haina kinga na alipangalo Mola hakuna mja anaweza lipangua ni semi ambazo hazina uhalisia katika mazingira ya barabarani na inachochea ajali zaidi kuendelea kutokea; tujipambanue kwa kutofanya makusudi na kupotezea kwa dai la ajali haizuliki kwa misemo hiyo ya kiswahili.



