Kutoka urithi wa kikoloni hadi mageuzi ya kikodi

KADRI Tanzania inavyoanza na kufanikiwa katika safari muhimu ya kufanya mageuzi katika mfumo wake wa kodi, kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo serikali na vyombo vyake inazivalia njuga kuliko wakati mwingine wowote.

Katika Baraza la 15 la Kitaifa la Biashara la Tanzania (TNBC) hivi karibuni, Rais Samia Suluhu alisisitiza haja ya kufanya mageuzi ya kina katika sekta ya kodi ili kushughulikia changamoto za ukosefu wa ufanisi, usawa, na ugumu ambao kwa muda mrefu umekuwa kikwazo kwa mfumo wa fedha.

Kimsingi, ingawa mfumo wa kodi nchini umebadilika kwa kiasi kikubwa katika miongo kadhaa, upungufu wake kimuundo na changamoto za kiusimamizi bado ni vikwazo vikubwa kufikia usawa wa kiuchumi na kuchochea maendeleo.
Makala haya yanajikita katika msingi wa kihistoria na hali halisi iliyopo sasa katika mfumo wa kodi Tanzania yakibainisha haja ya kufanyika kwa mageuzi makubwa sambamba na malengo ya maendeleo ya taifa.

Advertisement

Historia ya kikoloni na kodi kama chombo cha udhibiti mfumo wa kodi wa Tanzania inajitokeza kwa undani katika historia yake ya kikoloni, ambapo kodi ilikuwa chombo cha kudhibiti badala ya kuwa kichocheo cha maendeleo.

Enzi ya ukoloni wa Wajerumani (1885–1919) kodi mbalimbali ikiwamo ya kichwa iliwekwa kulazimisha wazawa kuingia kwenye uchumi wa fedha wa kikoloni. Kodi hizi ziliwalazimisha Watanzania ama kulima mazao ya biashara au kutumia nguvu zao kulipa kodi, mara nyingi kwa gharama ya kilimo cha kujikimu na maisha ya jadi.

Waingereza walipochukua udhibiti baada ya Vita vya Kwanza ya Dunia, waliendeleza na kupanua sera hizi kwa kuanzisha kodi ya kichwa kwa wanaume iliyolenga kuendeleza unyonyaji wa kiuchumi kwa wazawa. Ingawa kodi hizi zilileta mapato makubwa kwa utawala wa kikoloni, zilichochea umaskini na kuleta tofauti kubwa za kiuchumi zilizoendelea hata baada ya uhuru.

Mageuzi Baada ya Uhuru, ujumuishaji na maendeleo ya kitaifa Baada ya kupata uhuru mwaka 1961, Tanzania ilijitahidi kujenga mfumo wa kodi usio wa kinyonyaji na kuufanya ulenge kujenga taifa na uchumi. Katika mtazamo wa kijamaa wa Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Julius Nyerere, kodi zilikuwa njia kuu ya kugharamia elimu, afya na miundombinu.

Baada ya uhuru serikali ilitoa kipaumbele kuboresha usimamizi wa kodi kwa kuzingatia ukusanyaji wa mapato na usambazaji wake kwa usahihi. Kodi za kilimo zilikuwa nguzo muhimu ya mfumo mpya, zikitumia uchumi wa kilimo wa Tanzania kugharamia huduma za umma.

Hata hivyo, njia hii iliweka mzigo mzito kwa wakulima wa vijijini, wengi wao walikuwa wanashindwa kwa umaskini. Sera za utaifishaji zilizotangazwa katika Azimio la Arusha mwaka 1967 zilibadilisha sura ya mfumo wa kodi na kuelekeza mzigo mkubwa wa kodi katika mashirika ya umma huku ikipunguza utegemezi wa michango kutoka sekta binafsi.