Tamasha la ‘Flying Family Choir’ kutikisa Dar Juni 29

DAR ES SALAAM: Kwaya ya Flying Family inayojumuisha waimbaji kutoka madhehebu mbalimbali ya kikristo wenye vipaji vya uimbaji imendaa tamasha maalum litakalowakutanisha Watanzania wakiwemo wadau wa muziki na familia zao ili kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji wa nyimbo zenye ufundi wa hali ya juu.
Tamasha hilo ambalo litaambatana na uchangishaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya muziki vya kwaya linatarajia kufanyia Juni 29, mwaka huu katika ukumbi wa Kardinal Rugambwa uliopo St Peter’s Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa makala hii, Kiongozi wa kwaya hiyo Innocent Fundisha anasema wamekuwa na shauku kubwa ya kuboresha huduma yao ya uimbaji kupitia upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya muziki kama vipaza sauti, spika, kinanda na vinginevyo.
Amesema kupitia tamasha hilo, wanaamini watafikia lengo hilo kwa msaada wa wadau mbalimbali na wapenda muziki wa Injili.
“Kwaya ya FFC imekuwa ikitambulika kwa uimbaji wa nyimbo za ‘Classical’, tunafanya tamasha hili lengo ni kukutana na wadau wetu ambao watapa fursa ya kusikiliza nyimbo nzuri ambazo tumeziandaa, pia wataweza kutuchangia fedha ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya muziki, niwaombe watu kujitokeza kwa wingi kuhudhuria kwani ni tamasha la aina yake lililoandaliwa kwa ustadi mkubwa,” amesema
Aidha Fundisha anasema kwaya hiyo inajivunia kujenga umoja na upendo kwa wakristu kwa kutumia muziki na kuweza kuimba pamoja bila kujali tofauti zao za kimadhehebu kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita sasa na kufanikiwa kuandaa matamasha makubwa nane yaliyowakusanya waumini na viongozi mbalimbali wa kidini na kiserikali chini ya mchungaji mmoja Yesu Kristo.
Fundisha anasisitiza kuwa wapenzi wa muziki mtakatifu wakifika katika tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 29, 2025 katika ukumbi wa Kardinal Rugambwa St Peter’s Oysterbay, jijini Dar es Salaam watapata kusikia kazi za watunzi nguli kama George Handel, Wolfgang Mozart, Johan Bach, Joseph Haydn, Felix Mendelson, Anthonio Vivald na wengine wengi.
Hata hivyo anasema pia wanatumia kazi za watunzi wazawa kama David Wasonga, John Mgandu, Egidius Mushumbusi na Mathias Msafiri bila kusahau tenzi za rohoni.
Pamoja na muziki mzuri siku hiyo kutakuwa na chakula na vinywaji vya kutosha kwa washiriki wote kama sehemu ya kufurahia
Fundisha anasema si kazi rahisi kwa wanakwaya kujifunza nyimbo hizo lakini kwa msaada wa Mungu wanafanikiwa kushika na kujifunza kwa usahihi.
“Kwaya hii ilianzishwa Aprili, 2018 jijini Dar es Salaam ikiwa na wanakwaya wasiozidi 15 ila kwa sasa ina wanachama hai 40, tumeamua kumsifu Mungu na kutangaza sifa zake hapa duniani kwa njia ya uimbaji na kutumia muziki kudumisha umoja wa madhehebu ya kikristu,” anasema Fundisha.
Anasema anatambua kuwa tamasha hilo litawaleta pamoja ndugu, jamaa na marafiki hivyo anaamini kupitia tamasha hilo watu wataburudika, watafurahi kwa kusikiliza muziki wa classical.
Fundisha anasema lengo la kuanzishwa kwa kwaya hiyo ni kuleta umoja na mahusiano mazuri katika madhehebu ya kikristo kwa njia ya kushirikishana vipaji vya kimuziki.
“Tunashirikishana vipaji hivyo vilivyopo kwa kuandaa kwaya ya pamoja, matamasha mbalimbali, huduma kwa wahitaji pamoja na kushiriki matukio ya kijamii yanayolenga kudumisha umoja wa wakristu na taifa kwa ujumla,” anasema Fundisha.
Anasema kwaya hiyo imeunda bodi ya wadhamini yenye wajumbe tisa wenye jukumu la kusimamia utendaji wa kwaya, kupanga mikakati ya Kwenda mbele zaidi na kuhakikisha malengo ya kwaya yanakuwa endelevu.
Anasema Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Eng. Anastas Mbawala, Dk. Emmanuel Manase, Chancellor Fr. Dr. Vincent Mpwaji, Mama Rose Rupia, Rev. Boniface Kombo, Vicar General Fr. Richard Kamenya, Fr. Michael Ndawile, Prof. Alex Makulilo na Mama Miriam Solomon
Anasema kwaya inafanya mazoezi mara moja kwa wiki siku ya jumapili kuanzia saa tisa alasiri hadi saa kumi na mbili jioni, ili kutoa nafasi kwa wanakwaya wake ambao kila mmoja wao anahudumu kwenye kwaya yake kwenye usharika au parokia anakotokea na wanafanya mazoezi Katikati ya wiki na kuhudumu jumapili asubuhi.
“Hivyo kuimba kwenye kwaya ya Flying Family haimaanishi kuacha kuhudumu kwenye kwaya za kanisa anakotokea mwanakwaya,” alisema.
Aidha anasema sehemu kubwa ya mazoezi yanafanyika kwa njia ya mtandao wa WhatsApp ambapo kila sauti ina kundi lake na walimu wa kuwasimamia siku zote za wiki na jumapili inakuwa ni siku ya kuunganisha tu.
“Mwalimu anajirekodi na kuwatumia, kisha kila mwanakwaya anasikiliza na kujifunza na kisha kujirekodi na kutuma tena kwenye group kwa ajili ya mwalimu kusikiliza na kurekebisha. Kwa sasa tumeenda mbali zaidi ambapo nyimbo nyingi wanakwaya wanasikiliza wao wenyewe kupitia mtandao wa Youtube.
“Kisha mwalimu wa kila sauti hukutana na kundi lake kwa ajili ya masahihisho kabla ya kwaya nzima kukutana na kuunganisha siku ya jumapili. Kwaya ina walimu kumi na moja wenye uwezo mkubwa wa kusoma muziki, kupiga kinanda na piano, utunzi wa kiwango cha juu kabisa pamoja kufundisha somo la muziki kwa wanakwaya na wasio wanakwaya,” anasema Fundisha
Anasema yote hayo yanafanyika chini ya kikosi imara cha wataalamu kikiongozwa na Mwalimu Mathias Msafiri, CPA Innocent Fundisha, Egidius Mushumbusi, Jerry Newman, Eng. Deogratias Ngereza, Ainamringi Foya, Eng Pauline Tumaini, Lucy Mutongore, Elizabeth Malenga na Eng. Patrick Mamsery.
Fundisha anasema matarajio ya kwaya hiyo ni kutambulika na kuheshimika kimataifa kupitia kiwango cha juu kabisa cha ubora wa muziki na matamasha yake na kwamba hayo yote yatatokana na mipango sahihi ya kujutuma na nidhamu ya hali ya juu katika kuishi malengo ya kwaya.
Anasema wanawashauri vijana kutumia muda na vipaji vyao kumtukuza Mungu kwani ndiye aliyewapa vyote walivyo navyo.
Fundisha anasema kupitia vikundi vya uimbaji wanamtukuza Mungu na kupata wasaa wa kuepuka kushiriki vitendo viovu huko mitaani hivyo upata baraka na neema kwa kufanya yampendezayo Mungu.
“Tunatoa wito kwa wakristo wote kutambua kuwa sisi sote ni kondoo na mchungaji wetu ni mmoja Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo yatupasa kuishi kwa umoja na mshikamano na inawezekana kushirikiana bila kujali tofauti zetu za kimadhehebu.
“Lakini pia tunatoa wito kwa wenye vipaji vya kuimba au kupiga vyombo vya muziki wajiunge nasi kwa kufuata taratibu watakazopewa ili kudumisha umoja huu na kuueneza kwa wengi zaidi,” anasema
Hata hivyo anasema wanawashukuru wadau mbalimbali hasa walezi wao ambao ni maaskofu, wachungaji, mapadre pamoja na waamini kwa kuwapa moyo, kuwaongoza na kuwashauri, kuwawezesha kwa hali na mali bila kuwasahau watu binafsi na taasisi kama Paones General trading ambao wanawafadhili kwenye matamasha yao.