VIONGOZI wa mila jamii ya Kimasai ‘Laigwanani’ ni miongoni mwa watu wanaotumika katika kuhamashisha wananchi wa jamii hiyo ya kifugaji katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha kujiandikisha katika daftari la kupiga kura.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli na kusema kuwa asilimia 95 ya wakazi wa Longido ni wafugaji wa Kimasai na ili uweze kufanikiwa katika zoezi hilo lazima ushirikishe viongozi wa Milla ambao jamii hiyo inawaheshimu.
Kalli amsema yeye kama kiongozi mkuu wa serikali katika wilaya hiyo amezunguka,vitongiji 176,vijiji 51, kata zote 19 za Longido na kukutana na Malaigwanani na kuwaeleza umuhimu wa wao kujiandisha katika daftari la kupiga kura lengo likiwa moja tu kuhamashisha jamii hiyo ya kifugaji kujiandikisha.
Amesema mtaji wa maendeleo ni kujiandikisha katika daftari la kupiga kura hivyo hamasa katika wilaya yake ni kubwa na mwitikio wa watu kujiandisha ni mkubwa sana na anaimani zoezi la uandikishaji litafanikiwa kuvuka malengo ya uandikishaji katika Wilaya ya Longido.
Akizungumzia raia kutoka nchi jirani kuingia nchini na kujiandisha kwa kuwa wilaya yake iko mpakani, Mkuu wa Wilaya amesema ndio maana ameshirikisha viongozi wa mila, mabalozi na viongozi wa vitongoji na vijiji kwani ndio wanaoishi na watu hivyo raia hao hawatakuwa na nafrasi hiyo na wakifanya hivyo dola itawatia hatiani.
Mkuu wa Wilaya amesema kushirikisha viongozi hao wa vitongoji na vijiji kunaweza kuthibiti watu kutoka nje kuja Longido kujiandikisha katika daftari la kupiga kura hivyo uthibiti uko mzuri na wanaojiandikisha wanajuana makazi yao.
‘’Hapa kwangu niko vizuri sana katika zoezi la uandikishaji kwa kuwa nimeshirikisha viongozi wa Milla Malaigwani katika kuhamashisha uandikiishaji,”amesema Kalli
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido, Nassoro Shemzigwa amesema kuwa kila kitu kinaendelea vizuri katika zoezi la uandikishaji na hakuna changamoto yoyote hadi sasa iliyojitokeza juu ya suala zima la uandishaji.
Shemzigwa amesema hamasa imekuwa kubwa ya uandikishaji kwa wakazi wote wa wilaya ya Longido na hilo limefanikiwa baada ya jamii nzima ya kifugaji kutambua umuhimu wa kujiandisha katika daftari hilo.
Naye Diwani wa Kata ya Longido Mjini,Thomas Ngobei,Diwani wa kata ya Sinya,Seremoni Laizer na Diwani wa kata ya Olmolog Lomoni Mollel wote walisema zoezi la uandikishaji linaende vema na wakazi wa kata hizo wamejitoa na na huenda kata zao zikavunja malengo.