LATRA yashughulikia changamoto taxi mtandao

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Habibu Suluo, amesema wanaendelea kushughulikia changamoto za huduma za teksi mtandao, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na madereva na kampuni za teksi mtandao nchini.

Saluo amesema leo katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari kuwa mazungumzo hayo yanafanyika, baada ya kampuni za mifumo ya teksi mtandao za Bolt na Ubber kusitisha baadhi ya huduma za usafiri wa teksi mtandao, kutokana na kutoridhika na kiwango cha ukomo cha kamisheni cha asilimia 15, wanayopaswa kuwatoza madereva husika.

Amesema kati ya Septemba 5-8, mwaka huu, mamlaka ilifanya vikao na Chama cha Madereva wa Teksi Mtandao Tanzania (TODA), kampuni za Bolt na Ubber, ili kubadilishana taarifa na hoja za kibiashara na kiuchumi, ili kusaidia kampuni za mifumo ya teksi mtandao, madereva na abiria kupata huduma bora, endelevu na kwa thamani halisi ya fedha.

Advertisement

“Kufuatia vikao hivyo, mamlaka imeona itoe taarifa kwa umma kwamba vikao vyetu na mazungumzo yetu na TODA, Bolt na Uber yalikwenda vizuri.

“Kuna taarifa ya maandishi tunasubiri tupate leo na si zaidi ya kesho kutoka kwa Bolt na Uber, ili na sisi tukamilishe taratibu zetu za ndani kabla hatujatangaza rasmi maamuzi ya mamlaka,” amesema.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa mujibu wa Sheria Na. 3 ya mwaka 2019 ilitangaza viwango vya nauli za teksi mtandao kupitia Gazeti la Serikali Na. 1369 la tarehe 8 Aprili, 2022 na vyombo vingine vya habari.

Ameshukuru uongozi wa TODA na watoa huduma wa teksi mtandao walioendelea kutoa huduma, ikiwa ni pamoja na Paisha, Ping, Indrive na Little Ride.