LRCT, kuwafunda Wakurugenzi na Wakuu wa Idara za Halmashauri

KATAVI: TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imejipanga kutoa elimu ya Sheria kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara Katika halmashauri mbalimbali hapa nchini ili kuongeza uelewa juu ya mabadiliko mbalimbali katika sheria.

Naibu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Zainabu Chanzi amesema hayo alipokuwa akijibu maombi ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mifugo katika halmashauri hiyo, Tilinao Nsila.

Amesema moja ya majukumu ya Tume ya Kurekebisha Sheria ni kutoa elimu ya sheria hivyo utekelezaji wa ombi hilo utaanza mara moja kuzingatia bajeti pamoja na majukumu mengine ya tume.

Pia amesema Wakurugenzi na watumishi wengine ni wadau muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho taasisi inaendelea kukusanya maoni kwa ajili ya maboresho ya sheria mbalimbali.

“Katika halmashauri zetu Wakurugenzi ni wasimamizi muhimu wa sheria hivyo inafaa wapewe elimu kuhusu utekelezaji wa sheria mbalimbali ili kupunguza utendekaji wa makosa katika Jamii” amesema.

Awali alieleza kwamba sheria zinafanyiwa maboresho mara kwa mara na kuna baadhi ya sheria ambazo hazifahamiki kwa watu na viongozi ambao ndio wanaosimamia utekelezaji wa sheria na maendeleo ya wananchi katika ngazi za halmashauri.

“Naomba elimu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali zitolewe kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kuwa itasaidia utoaji wa huduma kwa jamii kwa kufuata sheria,” amesema.

Katika Mkoa wa Katavi wataalam kutoka tume hiyo wametoa elimu ya sheria ya makosa dhidi ya maadili,Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya, Makosa ya Kimtandao na Utakatishaji wa Fedha Haramu.

Mafunzo hayo yametolewa katika chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mpanda, Chuo cha Sayansi na Maendeleo ya Jamii Mpanda, vikundi vya waendesha bodaboda na bajaji, viongozi wa dini watendaji wa kata na wanawake wajasiriamali.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button