Lugha ya alama kujumuisha kwenye mtaala mpya

Serikali imepanga kuijumuisha lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini kwa lengo la kutatua changamoto ya mawasiliano zinazowakabili wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Deogratius Ndejembi ameliambia Bunge, jijini Dodoma leo asubuhi, mchakato wa mapitio ya sera na mitaala unaoendelea na somo hilo somo hilo limependekezwa kuwa la lazima.

Ametoa maelezo hayo baada ya Mbunge wa Viti Maalum Stella Ikupa Alex aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuingiza lugha ya alama kwenye Mitaala ya Elimu.

“Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa mpango na mapendekezo hayo, serikali imeandaa na kusambaza kamusi ya lugha ya alama ya Tanzania ya kidijitali katika shule na vyuo vinavyopokea wanafunzi viziwi.

“Aidha, kozi ya lugha ya alama ya Tanzania inatolewa katika chuo cha Ualimu Patandi na Kabanga na katika Vyuo Vikuu vya Dodoma, Dar es salaam na Archbishop Mihayo University, College Tabora (AMUCTA) kwa lengo la kumudu darasa jumuishi.

Ameongeza kuwa serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa walimu wa Elimu maalum na wasio wa elimu maalum 3,650 wa shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuwafundisha na kuwahudumia wanafunzi viziwi ili kujenga jamii jumuishi ya viziwi shuleni.

Habari Zifananazo

Back to top button