“Maafisa udhibiti ubora zingatieni sheria, weledi”

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Wilson Mahera.
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Wilson Mahera amewataka Maafisa Uthibiti Ubora wa Wilaya kutilia mkazo sheria, kanuni, na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Dk. Mahera ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo elekezi kwa Maafisa uthibiti ubora wa Wilaya wateule, yaliyoongozwa na kaulimbiu “Uthibiti Ubora wa Shule unaozingatia Weledi, Maadili na Uwajibikaji kwa Matokeo Chanya ya Ujifunzaji.”
Amesema ni muhimu kwa taasisi chini ya wizara hiyo kushirikiana kisekta ili kufanikisha mageuzi ya elimu nchini.
“Ufanisi katika sekta ya elimu unategemea ushirikiano kati ya idara mbalimbali zinazohusika na elimu, badala ya kufanya kazi kwa kutegemea wizara pekee,” amesisitiza Mahera.
Aidha, amewataka wathibiti ubora kutumia rasilimali chache walizonazo kwa ufanisi, akisema matokeo mazuri yataongeza thamani ya kazi zao na kuwapa fursa zaidi katika nafasi za juu.
Aidha Dk. Mahera amepongeza washiriki wa mafunzo kwa kujifunza masuala muhimu, ikiwemo Usimamizi wa utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa, uboreshaji wa kiunzi cha uthibiti ubora wa shule, matumizi ya mifumo ya NeST na SAS kwa manunuzi na usajili wa shule, taratibu za fedha na sheria za elimu.
Amesisitiza kuwa uthibiti ubora wa shule ni nyenzo muhimu ya kutathmini ufanisi wa shule na vyuo vya ualimu, akiwahimiza wathibiti kuendelea kujifunza kwa bidii hata nje ya mafunzo rasmi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule, Ephraim Simbeye, ameeleza kuwa wizara imefanikiwa kuboresha muundo wa Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule ili kwenda sambamba na mabadiliko ya mitaala.
Amewahimiza maafisa kulinda miundombinu na rasilimali walizokabidhiwa ili kukabiliana na changamoto za kazi.