Maamuzi kuhusu usalama wa nyama Vingunguti ni mazuri

KONGOLE serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kutengeneza soko la kisasa kwa ajili ya kuuza kitoweo cha nyama ya ng’ombe na mbuzi katika eneo la Vingunguti.
Natoa kongole kwa sababu moja na ya msingi kuhusu biashara ya nyama nchini ni mazingira safi kwa ajili ya afya za walaji.
Sheria ndogo inayoongoza machinjio inasema ni kinyume na utaratibu, machinjio ya wanyama kuwa sehemu ya soko ya mazao ya mifugo, hivyo kwa Jiji la Dar es Salaam kujenga soko nje kidogo ya machinjio ya Vingunguti kwa ajili ya manunuzi ni jambo la kupongezwa sana.
Soko hilo lenye vyumba 29 linahudumia ng’ombe 404 kwa wakati mmoja na mbuzi 300 kwa wakati mmoja, hii ni hatua muhimu iliyofikiwa na Halmashauri ya Dar es Salaam ikizingatiwa soko hilo lipo umbali wa mita 200 kutoka machinjio ya Vingunguti.
Japo matumizi ya soko hilo jipya na la kisasa lililoanza kutumiwa jana na wafanyabiashara wa nyama yalikumbwa na ukinzani hususani kutoka kwa wafanyabiashara wakisema gharama ni kubwa.
Wafanyabiashara hao wanadai ni gharama kutoa mifugo mnadani Pugu Dar es Salaam na kusafirisha hadi machinjioni.
Sanjari na hilo hulipa Sh 10,000 kwa kila ng’ombe mmoja anayechinjwa kisha kumsafirisha hadi soko jipya la nyama ambapo hugharimu Sh 5,000 na kisha kulipa Sh 5,000 ya ushuru katika soko hilo japo wamepewa kipindi cha mwezi mmoja cha matazamio.
Wanadai pia kujengwa kwa soko hilo kunasababisha nyama kuwa ghali kutokana na gharama za uendeshaji.
Hata hivyo, hatua zilizofanywa na Halmashauri ya Dar es Salaam inaonekana zimezingatia haja ya usafi na kuondoa mchanganyiko wa mambo katika shughuli inayohitaji usafi mkubwa ili kuleta usalama wa nyama.
Kutokana na umuhimu huo naona inafaa taratibu za soko hili zizingatiwe ili kuleta usalama wa nyama kutenganisha maeneo ya machinjio na mauzo.