MAANDALIZI kuelekea mbio za mwendo wa pole na haraka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Great Ruaha Marathon 2023) zinazotarajia kushirikisha wakimbiaji 500 kutoka ndani na nje ya nchi yanazidi kupamba moto.
Baadhi ya washiriki wanaoendelea kujiandikisha kupitia mitandao mbalimbali inayozitambulisha mbio hizo wametinga ndani ya hifadhi hiyo na kufanya zoezi la ukaguzi wa njia zitakazo tumika katika mbio hizo.
Mkurugenzi wa hoteli maarufu ya Mabata Makali Lodge and Campsite ambayo ni mmoja wa wadhamini wa mbio hizo, Eward Athanas amesema; “kitendo cha kukagua nacho kimekuwa cha kitalii sana na kinatarajiwa kuhamasisha utalii wa ndani.”
Mbio hizi zinazoratibiwa na Shirika la Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) kwa kushirikiana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA), zinatarajiwa kufanyika Julai 8, mwaka huu.
Mratibu wa mbio hizo kutoka shirika la SYDP linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya afya, stadi za maisha, ujasiriamali kwa vijana na hifadhi na utunzaji wa mazingira Hamimu Kilahama amesema Mbio hizo zitakazoanzia daraja la Mto Ruaha (Ibuguziwa), zitafanyika kwa umbali wa kilometa 5, 10, 21 hadi 42.
“Ili kuwezesha zaidi washiriki na wageni wengini kufurahia vivutio vya utalii katika hifadhi hii mbio hizi zitakwenda sambamba na matembezi ya kawaida hifadhini humo,” amesema.
Amesema dhumuni kubwa la mbio hizi kuhamasisha jamii kulinda vyanzo vya mto Ruaha Mkuu ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa wanyama wa hifadhi hiyo pamoja na kuhamasisha shughuli za utalii ndani ya hifadhi.
Alitaja malengo mengine ya mbio hizo kuwa ni pamoja na kusaidia kutangaza fursa za uwekezaji ndani na nje ya hifadhi, kuchochea ajira kupitia sekta ya utalii na hifadhi ya mazingira, na kuihamasisha jamii kushiriki vita dhidi ya ujangili.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Amina Rashidy amesema mbio hizo zinaenda kutoa fursa kwa wageni kuifahamu hifadhi hiyo, vivutio vya upekee vilivyopo pamoja na umuhimu wa mto Ruaha Mkuu ambao ni roho ya Hifadhi hiyo na shuguli zingine za kiuchumi ukiwemo uzalishaji wa umeme.
“Mto huu unaotegemewa kwa uzalishaji wa umeme unamwaga maji yake katika mabwawa ya kuzalishia umeme ya Mtera, Kidatu hadi Mwalimu Nyerere hivyo jamii ikieleweshwa umuhimu wake itachangia kuongeza wigo wa kutunza vyanjo vyake,” amesema.
Aidha alisema kwa kushirikiana na hoteli ya Mabata Makali Lodge and Campsite iliyopo nje ya hifadhi hiyo wamejipanga kupokea wageni na kuwahakikishia hali tulivu ya usalama kwani wana huduma ya vyumba vya kutosha na vyenye usalama wa kutosha kwa gharama za watu wa mtabaka yote.
Hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini baada ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere ipo kilometa 131 kutoka Iringa Mjini na ni maarufu kwa idadi kubwa ya Simba, chui, nyati, tembo, tandala wakubwa na wadogo, pundamilia, mbweha, fisi, mbwa mwitu, mamba, viboko, twiga, ndege zaidi ya 500 na aina mbalimbali za mimea.
Mmoja wa wadau waliojitokeza kushiriki mbio hizo,Eda Msafiri amesema; “nimejitokeza kushiriki mbio hizi nikitambua umuhimu wake katika kukuza shughuli za uhifadhi na utalii lakini pia kwa faida ya afya yangu kwani najua mazoezi ni afya.”
Aliomba wadau kuendelea kujiandikisha kwa kupitia waratibu wa mbio hizo huku akizihamasisha kampuni na taasisi zingine kujitokeza kuzidhamini ili kuziongezea hamasa zaidi.
Naye Magdalena Christian ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika kipindi kifupi kilichobaki ili waendelee kuandika historia ya ushiriki wao katika kampeni zinazohusu uhifadhi na utalii nchini.
Mwisho.