Maandalizi ‘Great Ruaha Marathon’ yashika kasi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kushiriki

IRINGA: Maandalizi ya msimu wa nne wa Great Ruaha Marathon yanaendelea kwa kasi kubwa huku tukio hilo linalojizolea hadhi ya kimataifa, likitarajiwa kufanyika Julai 5, 2025, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, mojawapo ya hifadhi kubwa na za kipekee barani Afrika.

Katika kuthibitisha uzito wa tukio hilo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, akiungana na viongozi wengine wakuu akiwemo Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, wawakilishi wa Benki ya Dunia, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Cosato Chumi.

Tukio hilo linaendelea kuwa jukwaa la kipekee la kuunganisha michezo, utalii, uhifadhi wa mazingira na afya, likiwa na lengo la kuchochea utalii wa Kusini, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira hususan vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu, pamoja na kujenga mshikamano baina ya wananchi na wadau wa maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha mbio hizo zinafanyika kwa usalama wa hali ya juu, amani na mafanikio makubwa.

“Mbio hizi ni tukio la kipekee linalopaswa kutangazwa duniani kote. Ni nadra sana kwa binadamu na wanyama pori kushiriki anga moja kwa amani katika mazingira ya asili. Hili ni jambo la kipekee linaloinua sura ya utalii wetu,” alisema RC James huku akiipongeza kamati ya maandalizi kwa kazi kubwa na nzuri.

SOMA ZAIDI

Watanzania waalikwa mbio za Great Ruaha

Kwa mujibu wa Mratibu wa Great Ruaha Marathon, Hamim Kilahama, usajili unaendelea vizuri na mwitikio wa washiriki ni mkubwa kuliko ilivyotarajiwa.

Alieleza kuwa mbali na mbio hizo, kutakuwa pia na vivutio vingine vya kipekee vya kiutalii kama vile sport fishing, safari za picha (game drive) na matembezi ya asili.

“Great Marathon si tukio la kawaida – ni sherehe ya kipekee ya utalii, mazingira na afya. Tunawakaribisha Watanzania na wageni kutoka ndani na nje ya nchi kuja kushuhudia na kushiriki katika historia ya aina yake,” alisema Kilahama.

Akifafanha kwanini Great Ruaha Marathon ni ya Kipekee, Kilahama amesema kwa kufanyika ndani ya hifadhi ya taifa, linaloifanya kuwa mojawapo ya mbio chache sana duniani zinazofanyika katikati ya pori la wanyama.
Lakini pia amesema mbio hizo zinalenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, hasa maeneo yanayohifadhi vyanzo vya maji muhimu kama Mto Ruaha Mkubwa.

Lakini pia amesema zinachochea utalii wa ndani na nje, na kuchangia pato la taifa kupitia sekta ya utalii, na zinawashirikisha viongozi wa kitaifa na mashirika ya kimataifa, jambo linaloipa uzito na hadhi ya kimataifa.

Huku dunia ikitazama Tanzania kama kitovu kipya cha mbio za mazingira, amesema Iringa inajiweka katika ramani ya dunia kama mwenyeji wa mojawapo ya matukio muhimu ya kiutalii na kimichezo.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Google pay 145$ dependably my last pay check was $8500 working 10 hours out of reliably on the web. My undeniably young family mate has been averaging 16k all through ceaseless months and he works around 24 hours dependably. I can’t trust in howdirect it was once I endeavored it out.This is my basic concern…HERE……… ­­W­­w­­w­­.­­J­­o­­i­­n­­S­­a­­l­­a­­r­­y.­­­C­­­o­­­m­­­

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button