Mabadiliko sheria ya uchaguzi, vyama vya siasa yasisitizwa

DAR ES SALAAM: Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ameitaka serikali kufanya mabadiliko katika sheria za uchaguzi na vyama vya siasa ili kuimarisha uwajibikaji wa viongozi na kuhakikisha sauti za wananchi zinasikilizwa.

Ameeleza hayo Januari 03, 2024 katika ufunguzi wa mkutano maalum wa baraza la vyama vya siasa uliofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Pia amesisitiza umuhimu wa amani na utulivu, ameeleza kuwa msingi wa amani ni haki, na hivyo kuna haja ya sheria imara zenye kulinda haki za wananchi. Pia, amegusia suala la ruzuku kwa vyama vya siasa, akipendekeza kugawanya 10% ya bajeti ya ruzuku kwa vyama vyote kwa usawa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, amethibitisha kuwa maoni ya wadau hayatakuwa na upendeleo. Hata hivyo, ameongeza kuwa falsafa ya 4R (Reconciliation, Reform, Rebuilding, and Revitalization) inapaswa kutekelezwa kikamilifu ili kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa.

Katika hatua nyingine Katibu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia nguzo mama ya “Reforms,” akionya kuwa bila mabadiliko, falsafa yote itapoteza maana.

Hotuba hizi zimepokelewa kwa uzito na wadau wa siasa na sheria, huku wengi wakiona kuwa ni hatua muhimu kuelekea maendeleo na uwajibikaji zaidi. Maoni hayo yana lengo la kuchangia  mustakabali wa taifa.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button