Mabilioni pesa kuboresha usafiri jiji la Dar es Salaam
Mwendokasi mpaka Bandarini

SERIKALI imetangaza mkakati wake wa kuboresha usafiri katika jiji la Dar es Salaam, kwa kuendeleza mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (DART)
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza leo Juni 24 jijini Dar es Salaam, Msigwa amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya jiji la Dar es Salaam, wameanza utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi barabara ya mabasi yaendayo haraka na utahusisha kilometa 24.3.
Amesema mradi huo utatoka katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto ambapo ujenzi wake unaendelea na mradi utagharimu shilingi bilioni 342.9.
Amesema, awamu ya nne ni ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka kutoka katikati ya jiji hadi Tegeta pamoja na kipande cha kutoka Mwenge hadi Ubungo, mradi huu upo katika hatua ya manunuzi
Aidha, amesema awamu ya tano ya ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka itahusisha kilometa 27.6 kutoka Ubungo hadi bandarini kupitia barabara ya Nelson Mandela pamoja na kipande cha Segerea hadi Kigogo.
“Awamu ya sita ya ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka utakua ni kutoka Morocco hadi Kawe kupitia barabara ya Mwai Kibaki, Kimara hadi Kibaha na Mbagala hadi Vikindu kilometa 26.5.; …. “Ni mradi mkubwa na tunatarajia utagharimu shilingi bilioni 603.8.” Amesema Msigwa