Mabondia wajiandae kwa ndondi za Dubai

TIMU ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa inatarajia kushiriki mashindano ya ngumi ya dunia yatakayofanyika Dubai, Falme za Kiarabu mwezi ujao.
Mashindano hayo makubwa yanaandaliwa na Chama cha Kimataifa cha Ngumi (IBA) na yatafanyika kuanzia Desemba 2 hadi 13, 2025 yakishirikisha mabondia wa nchi mbalimbali duniani wenye majina makubwa.
Viongozi wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), wamesema watapeleka mabondia katika mashindano hayo yatakayoshirikisha mabondia maarufu wanaume.
SOMA: Mabondia wajitosa kutangaza utalii
Mabondia wa Tanzania wajiandae vizuri kwa ajili ya mashindano hayo yanayotoa zawadi nono kwa washindi wa medali ya dhahabu, fedha na shaba watakaoshinda katika kila uzito.
Michezo ni ajira, michezo ni biashara kubwa sasa duniani na pia michezo ni afya inayosaidia watu kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na mengine ambayo husumbua watu wengi duniani.
Viongozi wa BFT wajitahidi kuwapa taarifa mabondia kuhusu mashindano hayo ya Dubai mapema na faida yake, Mara nyingi, viongozi wa mashirikisho mengi ya michezo husubiri siku zikibaki chache ndio hutoa taarifa kwa mabondia kuanza maandalizi.
Ni wazi mabondia wengine wanatoka katika taasisi za kijeshi, hivyo inabidi wapate ruhusa kutoka kwa mwajiri wao na wengine wanafanya shughuli zao, lazima waziweke sawa.
Hivi karibuni, timu ya taifa ya ngumi ya Tanzania ilishiriki mashindano ya Kanda ya Tatu ya Afrika yaliyofanyika Nairobi, Kenya na kumaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa ujumla mabondia wa Tanzania walifanya vizuri.
Mabondia hao wa Tanzania wanaonekana wako vizuri, hivyo waongeze mazoezi kujiandaa na mashindano hayo makubwa zaidi ya Dubai yatakayoshirikisha mabondia wengi nyota.
Washindi wa medali katika kila uzito ni kwamba atakayepata medali ya dhahabu atapata Dola za Marekani 300,000 (ambazo ni zaidi ya Sh milioni 800), medali ya fedha Dola za Marekani 150,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 400) na medali ya shaba Dola za Marekani 75,000 (sawa na Sh milioni 183).
Kwa kawaida, katika ngumi nafasi ya tatu, yaani washindi wa medali ya shaba huwa wawili, hivyo washindi wawili ya medali ya shaba kila mmoja anapata Dola za Marekani 75,000 (sawa na Sh milioni 183). Mshindi wa tano atapata Dola za Marekani 10,000 (sawa na Sh milioni 24.2).
Kwa hiyo, mabondia waanze maandalizi mapema wakianzia na yale ya nje ya kambi ya kudumu na viongozi wa BFT wajipange kuiweka timu katika kambi ya kudumu kwa maandalizi zaidi.
Zawadi hizo zitatolewa kwa mpango ufuatao, yaani bondia atapata asilimia 50 na kocha wake atapata asilimia 25, shirikisho lake la ngumi la nchi anayotoka litapata asilimia nyingine 25 iliyobaki.
Kuonesha michezo ni ajira kubwa, hivi karibuni mwanariadha Alphonce Simbu alishinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Riadha ya Dunia yaliyofanyika hivi karibuni Tokyo, Japan na alipata kitita cha Dola za Marekani 70,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 171).



