Machungu ya ‘chagulaga’ kwa mabinti wa Kisukuma

MILA ya ‘chagulaga’ kwa kabila la Kisukuma ambayo baadhi ya wadau wa maendeleo wanaiita kandamizi kwa watoto wa kike, sasa imebadilisha mtindo wa kuitekeleza.
Kwa tafsiri ya haraka, ‘chagulaga’ ni ‘chagua umpendaye’, mila ambayo miaka ya zamani, 1960 hadi 1990, ilikuwa ikitekelezwa baada ya kutawanyika kwa wanajamii waliokusanyika kwa ajili ya burudani na kubadilishana mawazo, ikiambatana na ngoma za jadi.
Wakati wa kutawanyika kwenye sherehe hizo, wanaume walijibanza sehemu kuwinda wachumba, kila mmoja kwa nafasi yake.
Wakati wa mkusanyiko, mvulana alichagua msichana na kumvizia popote wakati wa kurudi nyumbani, anamshika begani huku akieleza matamanio yake.
Upo wakati wanaume hata watano walichagua msichana mmoja, ikabidi kila mmoja kwa nafasi yake atafute nafasi baada ya mtawanyiko kunadi sera zake.
Pembeni anakuwepo mtu anayeona mchakato mzima, baada ya hapo anamshauri binti kuchagua mmoja kati ya waliojinadi ili mchakato wa posa uanze.
“Kwa hiyo chagulaga iliihakikishia utajiri familia yenye wasichana wengi, kwani tulikuwa tukitoa mahari hata ng’ombe 30 kwa binti,” anasema Mwenyekiti wa wazee wa Kisukuma mkoani Mwanza, Charles Masalakulangwa mwenye umri wa miaka 80 sasa.
Anasema waliokosa msichana ilibidi wakubali kushindwa, ingawaje wanaume wengine, akiwemo yeye, walikuwa wakikumbana na changamoto ya kukubaliwa na kisha kukataliwa baada ya siku chache msichana akigundua amechagua mwenye uchumi wa chini na kumuacha tajiri.
“Kilichofuata ni wao kufanya chagulaga katika maeneo mengine ya mkusanyiko wa wanawake, kama vile kisimani au msituni wanapotafuta kuni,” anasema Masalakulangwa.
Utandawazi sasa umebadili kila kitu. Nafasi ya ngoma za asili kama chanzo cha kukusanya Wasukuma kwa ajili ya burudani imeisha kwani wengi sasa wanapata burudani na taarifa kupitia runinga, redio na simu za mkononi, hivyo kukomesha mikusanyiko ya wanajamii.
Lakini pia Wasukuma wamekua wakisambaa katika mikoa mingine kutafuta maisha bora, ikiwemo Mkoa wa Katavi ambapo wameweka makao kwa wingi kwa shughuli hasa za kilimo na ufugaji.
Kila wanapopatikana kwa wingi wanaendeleza chagulaga kwa mtindo wa kulazimisha wasichana chini ya miaka 18 kuolewa, anasema Mkurugenzi wa asasi ya Usevya, Eden Wayiimba.
Asasi hiyo inayojishughulisha pamoja na mambo mengine kupinga ukatili wa kijinsia kwa wasichana na mimba za utotoni, imefanya uchunguzi na kugundua kwamba Wasukuma waliopo Katavi wanapomlazimisha binti kuolewa, asilimia kubwa ya wasindikizaji wa bibi harusi wanakuwa wa rika lake, ili kuwapa nafasi vijana kutekeleza chagulaga wakati wa sherehe hizo.
Wayiimba anasema hali hiyo ni kero kwa mabinti, inayowatia hofu na kuwafanya kukimbia hovyo hata kama ni usiku wa manane ili kuepuka ndoa za lazima.
“Chagulaga ina hasara lukuki kwa mtoto wa kike, ikiwemo kumnyima haki ya kupata elimu, lakini pia kumuingiza katika changamoto za ndoa na mimba za utotoni,” anasema.
Anawasihi wadau wengine kuunga mkono jitahada za kupinga ukatili wa kijinsia kwa mapambano endelevu hasa pale miradi ya wafadhili katika eneo husika inapofikia tamati.
Daktari wa magonjwa ya wanawake katika mojawapo ya hospitali mkoani Mwanza, ambaye hakupenda jina la taasisi yake litajwe, Jackson Mugyabuso, anasema mimba za utotoni ni hatari kiasi cha kusababisha vifo inapotokea mjamzito amekumbana na changamoto ya uzazi kinzani.
Anasema ni kutokana na kwamba viungo vya uzazi kwa binti havijakomaa kiasi cha kuruhusu kujifungua salama.
Kadhalika mimba za utotoni ni majawapo ya ugonjwa wa fistula, kutokana na sababu hiyohiyo ya viungo kutokomaa ipasavyo ili kuruhusu mtoto kupenya kirahisi.
Hali hiyo husababisha uchungu wa muda mrefu. Hali inakuwa mbaya zaidi kwa mjamzito aliye mbali na kituo cha afya kwani kuepuka fistula ni nadra kwake kutokana na kukosa usaidizi wa kitabibu wa haraka.
“Lakini pia mila kama hizo kandamizi ni chanzo cha magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo Ukimwi na kaswende kwani wahusika hawana muda wa kuchunguza afya zao kwanza,” anasema Dk Mugyabuso.
Ofisa katika Makumbusho ya Bujora ya kumbukumbu za kabila la Kisukuma mkoani Mwanza, Richard Bulluma anakiri kasi ya chagulaga kupungua kutokana na utandawazi, pamoja na maboresho ya huduma za kijamii, ikiwemo maji safi na nishati mbadala za kupikia, hiyo kuondoa mikusanyiko ya wanawake katika baadhi ya maeneo.
Anakiri kwamba chagulaga ni mila kandamizi, hasa inapomlazimisha msichana kuolewa na mwanaume asiye chaguo lake. Msichana aliyegoma kuolewa aliadhibiwa vikali ikiwemo kupigwa viboko hadharani.
Anasema aliyefikisha miaka 25 na zaidi bila kuolewa alipewa majina ya udhalilishaji, kama vile ‘nshimbe’, ikimaanisha yeye ni kahaba na mwenye maringo.
“Kwa upande mwingine chagulaga ilikuwa muhimu kwa sababu ilihusisha taratibu za wanajamii zaidi ya asilimia 80, kufurahi pamoja na kubadilishana mawazo,” anasema.
Mwanamke wa Kisukuma aliyeolewa kwa chagulaga, Emaculata Kabula ambaye ni mfanyabiashara mdogo katika soko la Mbugani jijini Mwanza, anaielezea mila hiyo kama mfumo dume unaomfanya mwanamke kushindwa kuendesha shughuli za kiuchumi, hivyo kuwa tegemezi kwa mume.
Anakumbuka pia jinsi mwanamke aliyekuwa na ajira yake, akalazimika kuacha kazi baada ya kuolewa, kama sehemu ya kumtii mume na kumpa nafasi ya kutambulika kama kichwa cha familia.
Emaculata anasema kibaya zaidi chagulaga inachochea ubaguzi kwani wasichana wanaochaguliwa kwa wingi ni wenye rangi nyeupe tu, weusi wanabaki.
Anasema anauona ubora wa chagulaga pale wachumba walipata muda wa kuchunguzana tabia kati yao lakini pia historia ya familia zao.
“Hii ilifanyika katika kipindi cha posa, ambacho taratibu za kupeleka mahari zilichukua muda mrefu,” anasema.
Anasema kwa kiasi kikubwa chagulaga ni mila yenye ubaguzi na ukandamizaji kwa mtoto wa kike kwani inamnyima nafasi ya ushirikishwaji na kutoa maamuzi katika masuala yote ya kijamii.
Anatoa pongezi kwa serikali na wadau wengine ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki za mtoto wa kike na wanawake, elimu ambayo imemsaidia yeye binafsi kuwa na ujasiri wa kuendesha shughuli zake za kipato.
Mhadhiri katika Idara ya Uandishi wa Habari Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Angelina Manyama ambaye pia ni Msukuma, anaona bado chagulaga ni muhimu kumfanya mwanamke kuwa karibu na familia kwa ustawi na makuzi bora ya watoto.
Anasema jukumu la kwanza na la msingi kwa mwanamke ni uangalizi wa karibu wa watoto, takwa analoweza kulitekeleza kwa ufasaha anapokuwa nyumbani wakati wote.
“Tofauti na sasa ambapo wanawake wametawaliwa na shughuli za kiuchumi na kusahau malezi ya watoto, hatimaye mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu,” anasema Angelina.
Tatu Bakari ni binti wa Kisukuma ambaye bado hajaolewa, kazi yake ni ususi wa nywele, anasema Chagulaga ni ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa inapomnyima msichana uhuru wa kuchagua mwanaume anayempenda kwa wakati wake mwenyewe.
Anasema kila Msukuma popote alipo aelimike, kwani utajiri hauletwi na ndoa za lazima bali kwa misingi bora ya maisha anayowekewa mtoto wa kike, ikiwemo elimu.
“Huenda kweli chagulaga imehamia mikoa mingine maana wazazi wangu hawaizungumzii. Wasichana tuko wanne kati ya watoto sita na wote tumeenda shule,” anasema Tatu.