Macron akutana EU kuijadili Ukraine

UFARANSA : RAIS wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amekutana na viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, katika mkutano wa kilele uliofanyika hivi karibuni.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuimarisha usalama wa Ukraine, hasa katika nyakati hizi za mzozo wa kivita unaoendelea na Urusi.
Katika mkutano huo, Rais Macron alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa kikosi cha Umoja wa Ulaya cha kusaidia Ukraine, ambacho kitakuwa na jukumu la kuimarisha usalama katika miji muhimu ya Ukraine.
Aliweka wazi kuwa pendekezo hili litaendana na makubaliano ya amani ya baadaye, na linaweza kutumika kujibu shambulizi lolote kutoka kwa Urusi.
Macron alieleza kuwa, licha ya kuwa Urusi inadai kutaka amani, inaendelea na mashambulizi ya kila siku dhidi ya ngome za Ukraine, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kiraia. “mashambulizi haya lazima yaishe, “alisema Rais Macron.
Aidha, Rais Macron pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, wamekuwa wakishinikiza kwa nguvu juhudi za kuunda muungano wa kimataifa ambao utaiwezesha Ukraine kupokea msaada wa kijeshi wa Umoja wa Ulaya.
Wakati mwingine, juhudi hizi za kimataifa zimekuwa zikikutana na changamoto kutokana na msimamo wa baadhi ya nchi kuhusu aina ya msaada unaotakiwa kutolewa.
Hata hivyo, viongozi hawa wawili wanaendelea na mashinikizo ili kuunda muungano imara wa mataifa kwa ajili ya kuleta amani ya kudumu Ukraine.



