Madaktari MOI kupewa mbinu matibabu ya mifupa

DAR ES SALAAM: MADAKTARI wa mifupa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) nchini watafundishwa mbinu za kisasa za matibabu ya majeraha ya mifupa lengo ni kuimarisha ujuzi.

Mpango huo ni baada ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Tiba ya Mifupa na Majeraha (IGTO) kukutana leo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya awamu ya 10 kuhusu mbinu mpya na za kisasa za matibabu ya majeraha na mifupa.

Akifungua rasmi mafunzo hayo leo Jumanne Mei 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk Mpoki Ulisubisya amesema ushirikiano kati ya MOI na Taasisi za Kinataifa umekuwa chachu katika kuwajengea uwezo madaktari wazawa na kuwapa mbinu mpya za kutibu majeraha na mivunjiko ya mifupa.

“Kwa mara ya 10 mkutano huu unaleta pamoja wataalamu kutoka nchi mbalimbali katika bara la Afrika, kwa ajili ya kujifunza mbinu mpya za kutibu magonjwa mbalimbali ya mifupa”

“Umoja huu umefanikisha matibabu yetu kuwa ya hali ya juu sana… Mivunjiko ya mifupa mingi ambayo zamani ilikuwa ngumu kuiunga lakini kwa sasa inatibika kwa urahisi,” amesema Dk Mpoki.

Aidha, Mwenyekiti mwenza wa IGTO, Profesa David Shearer ambaye pia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, amesema kuwa ana furaha kuwa nchini Tanzania na kushuhudia maendeleo makubwa yaliyofikiwa na MOI katika sekta ya mifupa pia amesema Tanzania ina wataalamu wenye uwezo mkubwa na wenye hamasa ya kujifunza, jambo ambalo limewavutia kama Taasisi ya IGOT.

“Ni furaha kubwa kuwa hapa Tanzania kwa mara nyingine tena, tumekuwa tukishirikiana na MOI kwa miaka kadhaa sasa na tunavutiwa sana na juhudi kubwa wanazofanya katika kutoa huduma bora na kuwa tayari kwa kujifunza,” amesema Prof. David

Naye, Mratibu wa mafunzo hayo, kutoka MOI, Dk William Mgisha ambaye pia ni daktari bingwa wa mifupa, amesema kuwa mafunzo hayo ni mfululizo wa awamu ya 10 tangu kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili, ambapo lengo ni kuwawezesha madaktari bingwa wa MOI na hospitali nyingine za rufaa nchini Tanzania na kupata mbinu mpya za upasuaji wa mifupa na mbinu bora za usimamizi wa majeraha makubwa.

Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo kutoka MOI, Dk Zakayo Wangwe, amesema mafunzo ni muhimu kwa sababu yanawaongezea ujuzi wa kitaalamu ambao unawasaidia kuboresha huduma wanazozitoa kwa wagonjwa katika maeneo yao ya kazi.

Mafunzo hayo yameanza  leo Jumanne Mei, 27, 2025 na yatafikia tamati Mei 30, 2025 katika ukumbi wa CHPE uliopo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button