Madarasa janja yanavyoleta mapinduzi ya elimu vijijini

MWANZA: MATUMIZI ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kupitia madarasa janja yaliyojengwa na Serikali yameanza kubadili mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji nchini, huku yakiwezesha mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wa shule zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Teknolojia hiyo imetekelezwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), unaohusisha ujenzi wa madarasa janja, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na kutoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi katika mikoa yote 26 nchini.

\kizungumza wakati wa ziara katika Shule ya Msingi Samia mkoani Mwanza, Dk Dugange alisema matumizi ya teknolojia hiyo yamerahisisha ufundishaji, kuongeza ufanisi wa walimu na kupanua fursa za wanafunzi kupata elimu bora bila kujali maeneo wanayoishi.

Alisema kupitia madarasa janja na vibao janja, mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wa shule tofauti kwa wakati mmoja, hatua inayosaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu.

Alisema wakati wa ziara hiyo alishuhudia mwalimu akifundisha wanafunzi wa Shule za Msingi Samia na Kanemwa, zilizopo katika kata tofauti, kwa wakati mmoja kupitia teknolojia hiyo.

“Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika sekta ya elimu nchini. Sasa ni jukumu la walimu na wazazi kushikamana kuhakikisha wanafunzi wanasoma vyema na kutunza miundombinu iliyopo,” alisisitiza.

Alisema mkoani Mwanza, kupitia mradi wa BOOST, zimejengwa shule 26 zilizochochea maendeleo ya wanafunzi, hususan katika matumizi ya TEHAMA.
Katika Shule ya Msingi Samia, alisema Serikali imetoa zaidi ya Sh milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 10 na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
KIGONGO YANUFAIKA

Akiwa katika Shule ya Msingi Kigongo, wilayani Misungwi, Dk Dugange alikagua miundombinu iliyojengwa kwa gharama ya Sh milioni 141, ikiwemo darasa janja na darasa la kisasa la elimu ya awali lililowekewa vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kufundishia.

Alisema maboresho hayo yameimarisha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufanisi wa wanafunzi katika masomo.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dk Fatma Mganga, alisema mradi huo umeleta maboresho katika sekta ya elimu kupitia uwekezaji wa miundombinu na teknolojia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Samia, Chacha Joseph, alisema shule hiyo imepatiwa darasa janja lenye kompyuta 20 na ubao janja mmoja.

Alisema vifaa hivyo vimeimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji, huku vikiwajengea walimu na wanafunzi uwezo wa kutumia TEHAMA katika shughuli za kielimu.

Aliongeza kuwa wanafunzi wanapata ujuzi wa msingi wa matumizi ya kompyuta, kujifunza kwa njia ya kidijitali na kufanya mazoezi ya masomo mbalimbali.

Alisema katika Kata ya Idetemya pekee kuna shule 10 zilizojengwa kupitia mradi wa BOOST.
Alisema Mkoa wa Mwanza umeendelea kufanya vizuri katika sekta ya elimu licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi, huku mwaka jana ukishika nafasi ya pili kitaifa kwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Mwalimu wa TEHAMA katika Shule ya Msingi Kigongo, Silvano Pamba, alisema madarasa janja yamepunguza changamoto ya upungufu wa walimu kwa kuwezesha mwalimu mmoja kufundisha shule zaidi ya moja kwa wakati mmoja.
Alisema teknolojia hiyo pia imesaidia kuboresha taarifa za kiutumishi za walimu na kuongeza hamasa ya wanafunzi kujifunza.

WANANCHI WAIPONGEZA
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mkapa, Kata ya Igoma, Charles Mayela, alisema matumizi ya TEHAMA shuleni yameongeza uwezo wa wanafunzi na kuwaandaa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

“Dunia ya sasa inakwenda katika matumizi ya TEHAMA, tunamshukuru Rais wetu Dk Samia kwa kuliona hilo na kutuletea madarasa ya aina hii hapa shuleni,” alisema.

Mkazi wa Kigongo, wilayani Misungwi, George Ngole, alisema maboresho yaliyofanyika yamewawezesha watoto kusoma katika mazingira bora na kupata elimu yenye ubora unaolingana na ile inayotolewa mijini.

Alisema matumizi ya mtandao katika ufundishaji yamepunguza usumbufu kwa walimu na kuwapa wanafunzi wa maeneo ya vijijini fursa ya kupata maarifa yanayopatikana kwa wenzao wa mijini.

Naye mkazi wa Kasene, wilayani Misungwi, Hellena Kafipa, alisema mradi huo umeondoa changamoto ya miundombinu duni ya madarasa kwa kujenga vyumba vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi.

Mwanafunzi wa Darasa la Tano katika Shule ya Msingi Kigongo, Witness Kigongo, alisema darasa janja limemsaidia kujifunza kwa haraka na kupata maarifa zaidi kuhusu matumizi ya TEHAMA.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button