Madereva TZ kushiriki mashindano ya magari Afrika

MOROGORO: MADEREVA 23 kutoka mataifa mbalimbali duniani wakiwemo Watanzania wamethibitisha kushiriki mashindao ya mbio za magari barani Afrika yanayofahamika kwa jina la ‘Mkwawa Rally of Tanzania’ ya umbali wa jumla ya kilometa 338.
Mbio hizo ambayo ni mzunguko wa mwisho wa kuwania ubingwa wa mashindano ya magari Afrika (ARC) (African Rally Championship) yamepangwa kuanzia Septemba 19 na kufikia tamati Septemba 21,mwaka huu mkoani Morogoro.
Msimamizi mkuu wa mashindano hayo, Dk Mosi Makau amesema hayo kuwa tayari madereva 23 wameshajisajili kushiriki , na mashindano hayo ni sehemu ya kuwania Ubingwa wa mashindano ya magari Afrika (ARC).
Amesema kuwa washiriki wengine wanapambania kombe la ndani ni baada ya kufanyika kwa mzunguko nchini Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Dk Makau amesema mashindano hayo ya mzunguko wa mwisho kwa mara ya kwanza yanafanyika mkoani Morogoro ambapo miongoni mwa madereva hao wanagombania taji la Afrika, wapo washindani wa ndani ambao nao wanajiandaa kugombania kombe la ndani la mashindano hayo.

Amesema mashindano hayo ya siku tatu na ufunguzi rasmi utafanyika Septemba 19 mwaka huu , na baada ya ufunguzi tayaendelea eneo la Tungi (Nanenane ) na Septemba 20 yatafanyika kwenye shamba la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) eneo la Mkundi kwa Makunganya na kuwepo kwa hatua tatu .
Dk Makau amesema hatua ya kwanza itakuwa mbio za kilometa 20, pili ni kilometa 12 na hatua ya tatu ni kilometa 30 na kwmaba kutakuwa na mizunguko miwili katika kila hatua moja na mashindano hayo yataendelea siku ya Septemba 21 katika eneo la TFS na kufanyika mzunguko mmoja .
“Kwa siku hizo tatu , jumla ya mashindano yatakuwa ni kilometa 338 , hivyo niwaombe wananchi Mkoa wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano,”amesema Dk Makau.
Dk Makau amesema mashindano hayo pia ni fursa kwa wakazi na wafanyabishara wadogo wa mkoa huo watafaidika kwa kufanya biashara zao kutokana na uwingi wa wageni wanaotoka nje ya nchi na ndani ya nchi kwa ajili ya kuja kushuhudia mashindano hayo.
Naye Mkurugenzi wa magari ya mashindano Tanzania, Satinder Birdi ametaja baadhi ya madereva wa magari 23 wengine ni kutoka nchi ya Uganda, Rwanda ,Burundi na India na wote hawa wanaingia Morogoro muda wowote kabla ya kuanza kwa mashindano.
Naye, Mwakilishi wa Mkwawa Group, Emmanuel Mhagama amesema kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na Wizara ya Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kukuza michezo nchini hususan mchezo wa mbio za magari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mount Uluguru Rally Club, Gwakisa Mahigi ambaye amebeba dhamana ya ulinzi wa mashindano hayo amewataka wadau na mashabiki wa mchezo huo kufuata maelekezo yatakayotolewa kwa lengo la kulinda usalama wao pamoja na usalama wa mchezo huo.
“Tumeshirikisha wenzetu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wakiwemo Askari wa Usalama Barabarani, Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kuweka huduma ya kwanza “ amesema Mahigi.



