Madini Tanzania na historia katika dhahabu, ajira na mapato lukuki

UWEKEZAJI katika sekta ya madini umeendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Kupitia sera bora na usimamizi madhubuti, sekta hii imechangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa kutokana na mapato yake mbalimbali.
Aidha, tozo, kodi, leseni na gawio kutoka kampuni za madini zimeiwezesha serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya huduma za jamii kama vile elimu, afya na miundombinu. Kimsingi, ongezeko la mchango wa sekta ya madini hadi kufikia asilimia 10.1 ya pato la taifa ni ishara ya mafanikio ya uwekezaji huu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, madini ni bidhaa ya kimataifa na usafirishaji wake pia huongeza fedha za kigeni ambazo ni muhimu kwa utulivu wa uchumi wa taifa. Mbali na mchango wa kifedha kwa serikali, uwekezaji katika sekta ya madini umekuwa na faida kubwa kwa ustawi wa kijamii, hasa katika maeneo yanayozunguka migodi.
Uchunguzi wa gazeti la HabariLEO umebaini kuwa, kampuni nyingi zinachangia ustawi wa jamii katika miradi ya mbalimbali ya maendeleo ya jamii kupitia mpango wa uwajibikaji wa kijamii (CSR) ikihusisha ujenzi wa shule, vituo vya afya, barabara na huduma za maji safi.
Hatua hiyo inaendelea kuboresha maisha ya wananchi na kutoa fursa kwa jamii kunufaika moja kwa moja na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Aidha, uwekezaji huo unaongeza ajira kwa Watanzania huku kampuni nyingi zikilazimika kuajiri wazawa kwa nafasi na biashara nyingi ikiwamo ya huduma na bidhaa mbalimbali jambo linalopunguza ukosefu wa ajira na kuongeza kipato cha jamii.
Kwa upande wa wawekezaji, sekta ya madini inatoa fursa ya faida kubwa kutokana na rasilimali nyingi zilizopo nchini. Kuwepo kwa mazingira bora ya kisera na kisheria yaliyofanywa na serikali kwa nyakati tofauti, ikiwemo Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania, kumeweka msingi imara kwa wawekezaji kuwekeza kwa usalama na uendelevu.
Imebainika kuwa, serikali imeboresha na kuimarisha utayari wa kushirikiana na wawekezaji kwa kutoa vivutio mbalimbali ikiwamo misamaha ya kodi kwa baadhi ya vifaa na teknolojia, pamoja na kuwa na mifumo ya mazungumzo ya mara kwa mara kati ya serikali na sekta binafsi kutatua changamoto zinazojitokeza hatua inayosaidia kuongeza imani ya wawekezaji wa ndani na wa nje kuwekeza nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini lililofanyika Ilemela mkoani Mwanza hivi karibuni, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde anasema sekta ya madini imeendelea kuleta manufaa ya kiuchumi nchini.
Anasema sekta hiyo imeongeza mchango wake katika pato la taifa hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka mmoja
kabla ya mwaka uliolengwa wa 2025 kufanyika kwa tathmini ya ongezeko hilo. Mavunde anasema hayo
ni mafanikio makubwa ya kujivunia kama taifa.
“Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024,” Mavunde anasema: “Sekta ya madini ilichangia Sh bilioni 753 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na Mwaka wa Fedha 2024/2025, Wizara iliwekewa lengo la kukusanya Sh trilioni moja ikiwa ni uchangiaji wa kuvunja rekodi ambao haujawahi kutokea katika sekta ya madini.”
“Zikiwa zimebaki siku 13 kufikia mwisho wa Mwaka wa Fedha (mwaka wa fedha umeisha jana, sekta ya madini mpaka leo tumeishaingiza katika Mfuko Mkuu wa Serikali Sh bilioni 985 zimebaki Sh bilioni 15 kabla ya mwaka kugeuka,” anafafanua na kuongeza kuwa, itafika Sh trilioni ifikapo Juni 30, mwaka huu (jana).
Anasema hatua hiyo inaandika historia na kudhihirisha kuwa, sekta ya madini ikisimamiwa vizuri inaweza kuleta mabadiliko chanya katika uchumi wa nchi. Kuhusu hifadhi ya dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anasema Rais Samia alitoa maelekezo mahususi kuhakikisha wizara inasimamia ipasavyo hifadhi au akiba ya dhahabu itakayonunuliwa kupitia BoT.
Anasema barani Afrika, nchi inayoongoza kwa kuwa na hifadhi ya dhahabu nyingi kupitia Benki Kuu ni Algeria ikiwa na tani 174 za dhahabu na nchi ya 10 katika kumi bora ni Msumbiji ikiwa na tani 3.984 ya hifadhi ya dhahabu.
Anasema Tanzania haikuwa nchi inayosomeka kwenye nchi zenye dhahabu katika Afrika, lakini mwaka jana Serikali ilifanya mabadiliko ya Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini ambacho kinawataka wamiliki wa leseni kutenga madini yasiyopungua asilimia 20 kwa ajili ya kuchakatwa, kuyeyushwa, kusafishwa na kufanyiwa biashara ndani ya nchi.
Anasema hatua hiyo imewezesha BoT kununua tani 5.2 za dhahabu na hivyo kuipiku Msumbiji katika nchi 10 bora Afrika katika kipindi hicho.
Imebainika kuwa, serikali inalenga kuhakikisha ndani ya muda mfupi ujao, Tanzania inaingia kwenye ramani kama moja ya nchi zenye hifadhi ya kutosha ya dhahabu itakayosaidia kuimarisha sarafu ya Tanzania zaidi ya Sh trilioni 5.3 zilitumiwa na kampuni kubwa za madini zilipo nchini kununua bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali katika sekta ya madini nchini katika mwaka wa fedha uliopita.
Anasema kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kupatikana kupitia uwekezaji huo, Watanzania wachangamkie fursa hizo kuhakikisha zinabaki nchini na zionekane katika maisha yao ya kawaida kwa kushiriki kutoa au kuuza bidhaa au huduma kwenye migodi nchini.
Anasema lengo lake kubwa ni kuhakikisha sekta ya madini inanufaisha mnyororo mrefu zaidi kwa Watanzania ili watu wengi wanufaike na rasilimali za madini zilizopo nchini. “Na ndio maana tunawataka Watanzania wachangamkie fursa hizo, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa sana endapo kitabaki kwenye uchumi wa nchi yetu,” anafafanua.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Madini, Dk Angeline Mabula anasema kamati inaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kuhakikisha rasirimali za madini zilizopo nchini zinawanufaisha Watanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya kuwashirikisha Watanzania katika Tume ya Madini, Theresia Numbi anasema kati ya mwaka 2018 na 2024 manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani yalitoka Dola za Marekani Milioni 756 mwaka 2018 na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.7 mwaka 2024 ya bidhaa na huduma zote na katika kipindi hicho ajira kwa Watanzania ziliongezeka kutoka wafanyakazi 6,668 hadi kufikia wafanyakazi 19,371.
I am now making an extra $19k or more every month from home by doing a very simple and easy job online from home. sxs I have received exactly $20845 last month from this home job. Join now this job and start making extra cash online by following the instructions on the given website………………….. Www.JoinSalary.Com