Madini ya betri, fursa ya viwanda Tanzania

TANZANIA inazidi kupata nafasi katika mnyororo wa kimataifa wa uzalishaji wa betri kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji wa graphite na madini mengine muhimu, huku ikikabiliwa na changamoto ya kuhakikisha sehemu kubwa ya thamani inayotokana na rasilimali hizo inabaki nchini.
Kuongezeka kwa shughuli za madini hayo kunaifanya Tanzania kuwa sehemu ya soko la kimataifa la malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa betri, lakini swali kubwa ni iwapo nchi itanufaika zaidi kwa kuuza madini hayo au itatumia fursa hiyo kujenga uwezo wa uchakataji na uzalishaji wa bidhaa za thamani kubwa.
Agosti 2026, Tanzania ilisaini makubaliano ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 100 na kampuni ya China ya Henan Yudi Mining kwa ajili ya mradi wa graphite mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa za S&P Global, Serikali inatarajiwa kuwa na umiliki wa asilimia 17 katika mradi huo, wakati kampuni hiyo ya China ikimiliki asilimia 83. Mradi huo unalenga kuzalisha takribani tani 50,000 za graphite kwa mwaka.
Uzalishaji wa graphite nchini pia umeongezeka kwa kasi, ambapo takwimu za U.S. Geological Survey (USGS) zinaonyesha uzalishaji uliongezeka kutoka takribani tani 13,500 mwaka 2023 hadi tani 38,140 mwaka 2024.
Hata hivyo, uzalishaji wa graphite ni hatua moja tu katika mnyororo mpana wa sekta ya betri.
Hatua zenye thamani kubwa zaidi zinaweza kujumuisha usafishaji wa madini, uzalishaji wa malighafi za betri, utengenezaji wa vifaa vya cathode na anode, utengenezaji wa seli za betri, urejelezaji wa betri na hatimaye utengenezaji wa magari yanayotumia umeme.
Utafiti wa kitaaluma uliofanyika mwaka 2026 kuhusu sekta ya madini muhimu nchini Tanzania umeainisha usafishaji wa malighafi za betri, uchakataji wa graphite na utenganishaji wa madini adimu kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kwa Tanzania kwa muda mfupi.
Hata hivyo, utafiti huo umebainisha pia changamoto zinazohusisha uwezo mdogo wa usafishaji, upungufu wa wataalamu wenye ujuzi wa kiufundi na mitandao ya wazalishaji wa ndani.
UZOEFU WA INDONESIA
Uzoefu wa Indonesia unatoa somo muhimu kwa Tanzania kuhusu namna ya kutumia madini kuchochea viwanda vya ndani.
Indonesia iliweka vikwazo katika uuzaji nje wa nickel ghafi kwa lengo la kuhamasisha uchakataji ndani ya nchi na baadaye kuvutia uwekezaji mkubwa katika viwanda vya kusindika nickel.
Hatua hiyo imeisaidia Indonesia kuwa miongoni mwa nchi zenye ushawishi mkubwa katika uzalishaji wa nickel duniani.
Hata hivyo, upanuzi wa haraka wa sekta hiyo umeambatana pia na changamoto za kimazingira na kijamii, ikiwemo athari zinazohusishwa na uchimbaji na uchakataji wa nickel.
Uzoefu huo unaonyesha kuwa kujenga viwanda vya uchakataji pekee hakuhakikishi kuwa nchi itakuwa na sekta endelevu ya uzalishaji wa betri.
Tanzania inaweza pia kukabiliwa na changamoto ya kuwa mzalishaji mkubwa wa madini yanayotumika katika betri huku hatua zenye thamani kubwa za uchakataji na uzalishaji zikifanyika nje ya nchi.
Mnyororo wa kimataifa wa uzalishaji wa betri tayari umejikita kwa kiasi kikubwa katika nchi chache. Indonesia imevutia uwekezaji mkubwa kutoka China katika sekta ya nickel, wakati Tanzania nayo inaendelea kupokea uwekezaji wa China katika sekta ya graphite.
Hali hiyo haimaanishi kwamba Tanzania itapoteza udhibiti wa rasilimali zake, lakini inaonyesha umuhimu wa kuangalia kwa makini muundo wa mikataba na uwekezaji katika sekta hiyo.
Miongoni mwa maswali muhimu ambayo Tanzania inapaswa kujiuliza ni nani atakayemiliki viwanda vya uchakataji, bidhaa zitakazozalishwa zitauzwa wapi, ni kwa kiwango gani teknolojia itahamishiwa kwa kampuni za Kitanzania na ni Watanzania wangapi watapatiwa ujuzi wa kuendesha viwanda hivyo.
Aidha, ni muhimu kujiuliza iwapo kampuni za Kitanzania zitaweza kushiriki katika uzalishaji wa malighafi za betri na baadaye katika utengenezaji wa betri wenyewe.
KUEPUKA KUBAKI MUUZAJI WA MALIGHAFI
Ili kutumia fursa hiyo, Tanzania inaweza kuhitaji mkakati wa muda mrefu wa madini yanayotumika katika utengenezaji wa betri unaounganisha uchimbaji na maendeleo ya viwanda.
Mkakati huo unaweza kujumuisha kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata graphite na nickel, kujenga vituo vya tafiti kuhusu malighafi za betri, kutoa mafunzo kwa wahandisi na wataalamu wa uchakataji wa kemikali pamoja na kuweka mazingira yatakayovutia wazalishaji wa vifaa vya betri.
Pia, mikataba mikubwa ya uwekezaji inaweza kuhusisha masharti ya uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, huku kampuni za ndani zikiwezeshwa kushiriki katika kusambaza bidhaa na huduma kwa sekta ya uchimbaji na uchakataji.
Uwezo wa urejelezaji wa betri nao unaweza kuendelezwa ili Tanzania isibaki katika hatua ya mwanzo ya mnyororo wa thamani.
Serikali pia imekuwa ikifikiria kuanzisha kituo cha ubora cha madini mkakati kinacholenga teknolojia ya betri na kuongeza thamani ya madini.
Kwa hiyo, fursa ya Tanzania ni kubwa zaidi ya kuuza graphite au nickel nje ya nchi.
Mtihani mkubwa ni iwapo utajiri wa madini utatumika kujenga msingi wa viwanda vya ndani vya kuzalisha malighafi za betri, vifaa vya betri na hatimaye betri, au Tanzania itabaki katika hatua ya mwanzo ya mnyororo wa kimataifa huku sehemu kubwa ya thamani ikiendelea kuzalishwa katika nchi nyingine.
Kwa Tanzania, kuongezeka kwa mahitaji ya madini muhimu kunapaswa kuwa fursa ya kuongeza thamani ya rasilimali, kujenga ujuzi wa ndani, kukuza viwanda na kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya manufaa ya mnyororo wa betri inabaki nchini.



