MADIWANI wa jiji la Arusha wamehoji ni kwanini watendaji wa jiji hilo wanakwamisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara na uwekaji wa mitaro.
Hatua hiyo ni kufuatia mvua kuanza kunyesha huku barabara za mitaani zikishindwa kupitika kutokana na mitaro ya maji kuziba.
Madiwani hao wametoa hoja hizo katika kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 na kuhoji juu ya fedha zilizotengwa Sh milioni 28 kwa kila kata kwa ajili ya kutengeneza miundombinu hiyo, na kutaka majibu kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Arusha ambaye ni Mganga Mkuu wa jiji hilo, Dk, Maduhu Nindwa.
Baadhi ya madiwani hao wakiwemo Alex Marti kutoka Kata ya Olasiti, Sakina Mpuju na Naboth Silasie Kata ya Lemara wakisema barabara za mitaani katika kata 25 na mitaa 154 ni mbovu ilhali vivuko vikiziba kutokana na uchafu na maji ya mvua kupitia juu ya barabara.
Diwani Naboth wa Kata ya Lemara na Isaya Doita kata ya Ngarenaro walihoji kwanini watendaji wa halmashauri wanakwamisha miradi ya maendeleo huku madiwani wakishindwa kueleweka kwa jamii
“Sisi ndio tunaona adha wanayopitia wananchi, kama kipindi hiki mvua zinavyoendelea kunyesha mitaro imeziba na barabara zinazidi kuharibika, wananchi wanashindwa kufanya shughuli zao kwa uhuru kwa sababu ya ubovu wa miundombinu, tunaomba majibu ya uhakika ya kuwapa wananchi wetu” wamehoji madiwani hao.
Awali akifungua baraza hilo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amewataka madiwani hao kutojadili suala la barabara kuwa, vifaa vimeagizwa vikifika wataambiwa.
“Vifaa vimeagizwa nje na vikiletwa tutaitana kuvipokea ili kazi ya matengenezo ya barabara na mitaro iendelee, bahati nzuri ukusanyaji wa mapato unaenda vizuri, hivyo ni imani yangu kwamba miradi yote itakamilika kwa wakati”