Madiwani Ilemela wataka fidia waliochukuliwa maeneo

BARAZA  la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza limemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, wakili Kiomoni  Kibamba kuhakikisha analipa fidia katika maeneo yote yaliyochukuliwa na manispaa hiyo kwa shughuli za utekelezaji wa miradi ya   maendeleo ili yaweze kumilikiwa na umma.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi Februari 01,2024 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo kujadili taarifa za utekelezaji katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023-2024 Oktoba hadi Desemba, Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo, Renatus Mulunga amesema upo umuhimu wa kutwaa maeneo kwa kulipa fidia na kuyalinda kwa ajili ya shughuli za umma.

“Niwapongeze na kuwashukuru viongozi waliokuwepo wakati Hayati Mwalimu Nyerere anatangaza vijiji vya ujamaa ambapo maeneo kama ya Sangabuye wakachukua eneo kubwa sana, wasingechukua maeneo makubwa hata ile sekondari ya Sangabuye isingekuwepo, Mkurugenzi tumia maarifa yako yote, uwezo wako wote, sheria zako zote hakuna kuachia hata kipande cha ardhi tulichokitwaa.”Alisema Mulunga

Advertisement

Aidha katika hatua nyingine Mulunga amewaasa viongozi wa halmashauri hiyo pamoja na maeneo mengine  kufikiria vizazi vijavyo pindi wanapopanga mipango ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo pamoja na kutanguliza maslahi ya umma badala ya kujifikiria wao binafsi ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na rasilimali za nchi zilizopo.

Akichangia mjadala huo, Wakili Wilbard Kilenzi ambaye ni diwani wa kata ya Ilemela alishauri baraza la madiwani la kuhakikisha linasimamia msimamo wa kutorejesha maeneo yaliyotwaliwa kwa shughuli za umma kwa kuwa kufanya kinyume chake ni kuiingiza Manispaa hasara kwani itapaswa kulipa gharama zaidi za fidia kwa waliotwaliwa maeneo yao kutokana na kuwasitishia kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu na hivyo kusisitiza juu ya suala la ulipaji wa fidia kwa maeneo hayo yaliyotwaliwa.

Baadhi ya madiwani kwa nyakati tofauti walishauri kuwa ni vyema halmashauri ikaweka utaratibu wa kutenga fedha kila mwezi kwa ajili ya malipo ya fidia ili kuondokana na deni hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela wakili Kiomoni Kibamba alifafanua hoja hiyo kwa kusema, kuwa zaidi ya shilingi bilioni 5.9 zinadaiwa na wananchi kwa ajili ya fidia kutokana na Serikali kutwaa maeneo yao kwa shughuli mbalimbali za maendeleo na kwamba Manispaa yake itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya fidia hizo na kusema kuwa kwa maeneo yote ambayo yameshapimwa hayatarudishwa kwa wananchi.

“Maeneo yote ambayo tulikwisha kuyapima hayatarudishwa aidha tunahitaji kuchukua maeneo zaidi na tayari nimemuelekeza Mchumi kuandika andiko la kuomba mkopo ili tuweze kuchukua maeneo zaidi, na halmashauri itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia na kuzidi kubuni vyanzo vya fedha ili kuweza kulipa deni lote la fidia”….Alifafanua Kibamba