HALMASHAURI ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara imekabidhi vishikwambi 50 kwa madiwani pamoja na wataalam mbalimbali kwenye manispaa hiyo vilivyogharimu zaidi ya Sh milioni 32.
Akitoa taarifa kuhusu vishikwambi hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tehama Athumani Mfaume amesema vishikwambi hivyo vitawezesha kuleta ufanisi katika utendaji wao wa kazi.
Hayo yamejiri leo Novemba 8, 2024 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa manispaa hiyo kuhusu kupitia taarifa mbalimbali za halmashauri robo ya kwanza mwaka 2024/2025 kilichofanyika kwenye manispaa hiyo.
‘’Lengo na dhamira ya manispaa ni kuwezesha ufanishi wa utendaji kazi wa madiwani na wataalama hususani kipindi cha vikao mbalimbali vya kisheria ili kuweza kufikishiwa taarifa ya vikao kwa ufanisi na haraka zaidi,’’amesema Mfaume.
Akizungumza leo wakati akifungua kikoa hicho cha baraza la madiwani hao, Meya wa Manispaa hiyo Shadida Ndile amewaagiza madiwani na wataalam hao kuwa, wasiende kutumia vibaya shikwambi hivyo katika matumizi binafsi kwani haitakubalika kinyume na hapo wakahifadhi nyaraka za serikali.
Amesema yoyote atakayebainika ametumia kishikwambi kutoa nyaraka za serikali bila utaratibu wowote atachukuliwa hatua za kisheria kwani lengo ni kuongeza ufanisi na kupunguza gharama ya matumizi ya halmashauri hiyo.
Diwani wa Kata ya Vigaeni kwenye manispaa hiyo, Saidi Nassoro ‘’Tunashukuru tumekabidhiwa vishikwambi jambo ambalo lilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa sisi madiwani na leo tumekabidhiwa tunawashukuru sana kwasababu itasaidia watu kusoma dekumenti kwa haraka lakini pia tumekubali kuvilinda ili rasilimali hizi za wananchi ili ziweze kuwa salama‘’