BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba hawajaridhishwa na utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kile kinachodaiwa kupuuzia hoja zinazowasilishwa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani.
Madai hayo wametolewa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa halmalmashauri hiyo, robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika katika halmashauri hiyo.
Diwani wa kata ya Nitekela katika halmashauri hiyo, Salumu Chihediwe amehoji taarifa ya kamati ya fedha kuhusu kiasi cha fedha kilicho kopwa kutoka kwenye kiwanda cha tofari kinachomilikiwa na halmashauri hiyo hasa matumizi na kiasi hicho kilicho kopwa.
Hata hivyo amemuomba mwenyekiti wa baraza hilo kupitia baraza kukaa kwa pamoja kumjadili mkurugenzi huyo ambae anakwenda kinyume na utaratibu wa utumishi.
“Sikubaliani na maagizo haya ya kamati ya fedha kwasababu maagizo yalipuuzwa ya kikao kilichopita.
Ameongeza kuwa, “Kikao hiki tunaagiza tena, naomba kupitia baraza lako kwa niaba ya wajumbe wenzangu huyu mtumishi hadi kikao cha kamati ya fedha hao watu wawe wameshalipwa hiyo fedha”.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Jamali Kapende amesema kupitia kikao cha kamati kilichojadili utendaji kazi wa mkurugenzi huyo wajumbe wamewaomba wenye mamlaka,dhamana ya mkurugenzi kwamba hawahitaji kufanya nae kazi kwa sababu hatoi ushirikiano kwa madiwani.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mtwara vijijini Didas Zimbihile amewaomba watunza kumbukumbu za vikao kutengeneza muhtasari wa kikao husika na kufikia maadhimio yanayotokana na kikao hicho ili yafanyiwe utekelezaji kwa wakati ili kuepusha mvutano na marumbano kwenye vikao vijavyo.
‘’Niwaombe watendaji, tuache kutegeana na badala yake kila mmoja atimize wajibu wake kwenye maeneo yake ya kazi kwa kutumia maarifa mliyonayo katika utendaji kazi ili tuweze kusaidia halmashauri yetu’’