Madiwani wakataa kugawa Jimbo la Arusha

ARUSHA; MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamekataa kuligawa Jimbo la Arusha.

Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranghe alisema hayo baada ya kumalizika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani kujadili mchakato wa kuligawa Jimbo la Arusha Mjini juzi.

“Madiwani waliokaa waliazimia kuwa hakuna kugawa Jimbo la Uchaguzi la Arusha Mjini, litabaki kuwa jimbo moja. Azimio la pili ikawa ni kugawanya baadhi ya kata, tulikubaliana kata nane zilizopo Kusini mwa Jiji la Arusha zigawanywe,” alisema Iranghe.

Aliongeza: “Kwa eneo la Jimbo la Arusha linatawalika vizuri na madiwani kwa pamoja wakapitisha azimio kuwa jimbo lisigawanywe mara mbili”.

Iranghe alisema eneo la halmashauri hiyo mwanzo lilikuwa dogo na walifanya jitihada za kuliongeza hivyo kwa sasa hawahitaji kuligawa mara mbili huku ukubwa wa jimbo hilo uliopo sasa unatosha kuwahudumia wananchi wake.

“Eneo la jiji zamani lilikuwa ni eneo dogo, kwa hiyo liliongezwa kwenda kilometa za mraba 272 ili lipate hadhi ya kuwa jiji, sasa tumepata halmashauri ya jiji leo tena tunarudi tunataka tugawe tupate halmashauri ya manispaa tukaona Hapana,” alisema.

Alisema madiwani wa halmashauri hiyo wamekubaliana kugawanya kata nane kutokana na changamoto katika kuwafikia wananchi na kushindwa kutatua kero kwa wakati kutokana na ukubwa wa maeneo hayo.

Iranghe alitaja kata zilizoazimiwa kugawanywa ni Muriet itakayogawanywa katika kata tatu, Sokoni I nayo kugawanywa katika kata tatu, Moshono, Sinoni, Lemara, Olasiti, Terrat na Unga Limited.

“Lengo ni kuhakikisha huduma inawafikia wananchi kwa urahisi… ukiangalia kata kama Muriet ofisi ya mtendaji ipo Kwamrombo ni zaidi ya kilometa 20 sasa utoke kilometa 20 kutafuta huduma kwa mtendaji wa kata inakuwa changamoto kidogo,” alisema meya huyo.

Aliongeza: “Lengo la serikali kupeleka shule kila kata maana yake shule sasa zitajengwa katika kata hizo mpya za Halmashauri ya Jiji la Arusha”.

Jana ilikuwa siku ya mwisho kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupokea mapendekezo ya kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi.

Februari 26, mwaka huu Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele alisema tume hiyo inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Namba 2 ya Mwaka 2024.

Jaji Mwambegele alisema vigezo vitakavyotumika ni wastani wa idadi ya watu, ambako kwa majimbo ya mjini ni kuanzia wastani wa watu 600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia wastani wa watu 400,000.

Alitaja vigezo vingine ni hali ya kiuchumi ya jimbo, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, uwezo wa ukumbi wa Bunge, idadi ya wabunge wa Viti Maalumu Wanawake, upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button