Madiwani wamchagua mwenyekiti halmashauri ya Longido

ARUSHA: MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido mkoani Arusha wamemchagua kwa kura zote 26 diwani wa Kata ya Longido Mjini, Thomas Ngobei kuwa mwenyekiti mteule wa halmashauri hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Pia huenda akapitishwa kuwa mwenyekiti kwani jimbo halina wagombea upinzani nafasi ya udiwani.

Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo Wilaya ya Longido, Solomoni Lekui uchaguzi huo ulipaswa kuwa na wajumbe 29 katika jimbo hilo lakini wajumbe 26 walikuwepo katika upigaji kura na wajumbe watatu hawakuwepo.
Hata hivyo hakuna kura iliyoharibika katika uchaguzi huo wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Lekui alisema katika uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido, wajumbe wa mkutano huo walimchagua Peter Lekanet kushika nafasi hiyo baada ya mgombea mwenzake Solomoni Kool kujiondoa na kumuunga mkono Lekaneti aliyepata kura zote 26.
Lekanet ambaye ni diwani wa Kata ya Tingatinga Jimbo la Longido naye akapitishwa kuwa Makamu Mwenyakiti kwa kuwa jimbo hilo hakukuwa na wagombea wa vyama vya upinzani nafasi ya udiwani.
Naye, katibu wa Siasa,Uenezi na Mafunzo wa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Amani Lendieni amesema kuwa jimbo hilo lilikuwa na wagombea watatu katika nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro na ManjaYaille amechaguliwa kwa mwenyekiti mteule kwa kupata kura 20 na kuwaangusha vibaya wapinzani wake.

Yaille mwenyekiti mteule wa Jimbo la Ngorongoro aliwaangusha wapinzani wake Mathew Mollel aliyeambulia kura 14 na Baraka Barasobian aliyeambulia kura 4 katika uchaguzi uliokuwa na ushindani wa hali ya juu hivyo wamekuwa wagombea katika uchaguzi wa vyama vingi.
Katika Jimbo la Meru Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, madiwani wa jimbo hilo wamemchagua Lucas Kaaya diwani wa kata ya King’ori kuwa mwenyekiti mteule wa jimbo hilo kwa kupata kura 21 na kumwangusha mwenyekiti wa zamani Jeremia Kishili aliyeambulia kura 15.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, madiwani wa wilaya hiyo wamemchagua Engelbert Qorro kwa kura 15 na kuwangusha vibaya wapinzani wake John Mahu aliyepata kura 6 na Peter Mmassy aliyeambuli ziro .
Kwa Mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Karatu Anas Msabaha alisema kuwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti alichaguliwa diwani Silili James kwa kura 15 na kuwaangusha wapinzani wake akiwemo Sabina Marmo aliyeambulia kura 4 na Bosco Bura aliyepata kura 2 na wapiga kura katika uchaguzi huo walikuwa 21 hakuna kura zilizoharibika.

