Maelezo yaja na mwongozo kuepuka chuki, kashfa

IDARA ya Habari – MAELEZO imeandaa mwongozo kwa vyombo vya habari uonavitaka viepuke maudhui ya chuki, ubaguzi, kashfa, matusi na kuchochea vurugu katika kuripoti Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Egbert Mkoko amesema mwongozo huo pia unawataka waandishi wa habari kuchapisha habari za kweli, sahihi na zinazoweza kuthibitishwa.

Dk Mkoko alisema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu mwongozo huo kwa niaba ya idara hiyo kwenye mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Dar es Salaam jana.

Mwongozo huo ulioandaliwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), umewataka waandishi kuepuka kubashiri matokeo, kupendelea na kueneza uvumi na madai yasiyothibitika.

Sambamba na hayo, Dk Mkoko alisema mwongozo huo unaotumika kwa vyombo vyote vya habari unavitaka vyombo vya habari kuweka uwazi katika vipindi na matangazo yaliyolipiwa na vyama vya siasa.

Kadhalika, alibainisha kuwa mwongozo unawataka waandishi wote watakaohusika katika kuripoti uchaguzi mkuu kuhakikisha wamepata ithibati kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).

Aidha, mwongozo huo unawataka wamiliki wa vyombo vya habari kutoa taarifa polisi na kwenye Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu aina yoyote ya vitisho, mashambulizi na usalama wa waandishi wake wakati wakitekeleza majukumu yao.

Dk Mkoko

Alisema mwongozo pia unaelekeza vyombo vya habari vilivyopanga kuendesha midahalo ya kisiasa vinapaswa kuhakikisha midahalo hiyo uendeshwaji wake unazingatia sheria za uchaguzi na kutoa nafasi sawa kwa wagombea.

Sambamba na hayo, muongozo unaelekeza vyombo vya habari kuwa vinapaswa kusitisha kuripoti mikutano ya kampeni saa 12 kabla ya muda wa kupiga kura ambapo katika kipindi hicho hairuhusiwi kurusha au kuchapisha matangazo ya kampeni, ujumbe wa kumuunga mkono mgombea au maudhui yoyote ya kisiasa kwenye magazeti, redio au televisheni au majukwaa ya kidijiti.

Mbali na hayo, mwongozo unaelekeza kuwa vyombo vya habari havitaruhusiwa kuwa na vituo vya kujumlisha matokeo na badala yake vitapaswa kuripoti matokeo rasmi kutoka Inec.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button