Mafanikio Simba yachomoza bungeni

DODOMA; KLABU ya Simba imepongezwa kwa kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na pia kushika nafasi ya nne kwenye viwango vya ubora Afrika.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2025/26.
“Mheshimiwa Spika, angurumapo simba mcheza nani? Nitumie fursa hii kuipongeza kilabu ya Simba kwa mafaniko makubwa waliyoyapata kwa kufanikiwa kufika katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
“ Mafanikio haya si tu yanatoa heshima kwa kilabu hiyo, bali pia yanaitangaza nchi yetu katika ramani ya soka la kimataifa. Kupitia mafanikio haya, Simba, imeweza kushika nafasi ya nne kati ya vilabu bora barani Afrika jambo ambalo ni fahari kwa nchi yetu.
“Aidha, huu ni ushahidi tosha kuwa sekta ya michezo ikipewa kipaumbele na uongozi wa juu wa nchi, inaweza kuwa injini muhimu ya maendeleo ya taifa letu.
“Pia, nitoe pongezi kwa mwanariadha mashuhuri na shupavu Alphonce Felix Simbu ambaye hivi karibuni aliipeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa kwa kushika nafasi ya pili katika Mashindano ya Mbio za Boston zilizofanyika nchini Marekani tarehe 21 Aprili 2025. Ushindi wake umeitangaza nchi yetu katika tasnia ya michezo ulimwenguni,” amesema Waziri Kabudi.