Mafinga moto mkali: Wagombea wamwaga sera, mshindi kupatikana kwa jasho

IRINGA: Mji wa Mafinga umekuwa kitovu cha kisiasa baada ya wagombea wa ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumwaga sera zao kwa mvuto mkubwa mbele ya wajumbe wa chama, kila mmoja akionesha dhamira ya kuibeba Mafinga kimaendeleo.
Aggrey Tonga: “Sitafuti nafasi, nataka maendeleo” Tonga aliteka hisia za wajumbe kwa kusisitiza kuwa anagombea kwa sababu ya dhamira, si maslahi binafsi. Alihoji kwa nini halmashauri yenye mapato makubwa bado inakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya maji na barabara.


“Wawekezaji wapo wengi, lakini jamii inanufaika kiasi gani? Ni lazima vijana wapate ajira zenye staha, na wawekezaji wazingatie sheria za kazi,” alisema.
Aliahidi ubunifu katika kilimo cha mazao mapya yanayokubali Mafinga, ujenzi wa kituo cha afya kipya, na uongozi shirikishi utakaowapa wananchi nafasi ya kumsahihisha pale inapobidi.

Dk Basil Tweve: “Nitakuwa sauti ya wasio na sauti”
Tweve alikumbusha ushindani wake mkali wa 2020 aliposhinda kura za maoni kwa tofauti ndogo, akiahidi kushirikiana na wananchi bega kwa bega.
Alilenga zaidi malalamiko ya malipo duni katika viwanda vya wachina, akiahidi kulinda maslahi ya vijana na kuendeleza maendeleo shirikishi.

“Luganga haiwezi kubaki nyuma huku wawekezaji wakilipa vijana malipo duni. Nipeni ridhaa, nitakuwa sauti ya wasio na sauti,” alisisitiza.
Dikson Lutevele “Villa”: Mageuzi kwenye miundombinu na michezo
Lutevele aliahidi kushughulikia changamoto za mawasiliano, maji na barabara ya Njiapanda-Isupilo, akilalamikia vumbi linalotesa wananchi.
“Ubunge ni taasisi, sio mali binafsi. Mkinipa nafasi, nitaboresha michezo kwa kuanzisha viwanja rasmi na kubadilisha baadhi ya maeneo wazi kuwa viwanja vya michezo,” alisema.
Cosato Chumi: “Maendeleo ni hatua”
Mbunge anayemaliza muda wake, Cosato Chumi, alijivunia miradi aliyoitekeleza ikiwemo umeme na mradi wa maji wa Sh bilioni 48.
Aliahidi kukamilisha yaliyosalia, kujenga kituo cha afya Luganga, na kudhibiti ukiukwaji wa haki za wafanyakazi viwandani.
“Tumejivunia misitu yetu kwa kutoa ajira nyingi kwa vijana, tutahakikisha sheria za kazi zinazingatiwa ipasavyo,” alisisitiza.
Kigola Mendrad: Ahadi kubwa ya afya na barabara
Mendrad alitoa ahadi ya barabara za lami kila mtaa na ujenzi wa hospitali kubwa itakayofanana na Hospitali ya Ikonda, wilayani Makete.
“Nataka Mafinga iwe kitovu cha huduma bora za afya na barabara za kisasa,” alisema.
Mwisho

