GEITA: CHAMA cha wazalishaji wa mbegu za viazi vitamu kanda ya ziwa (Chawavitamb-Kazi) kimejipanga kuja na muongozo thabiti utakaosaidia kuratibu mipango na mikakati ya kufikia mageuzi ya kilimo cha viazi.
Muongozo huo unaandaliwa kwa kushirikisha wadau wa kilimo cha viazi ambao ni Kituo cha Utafiti wa Viazi kimataifa (CIP) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ambapo wamekutana mjini Geita.
Ofisa Utafiti wa CIP, Saadan Amon amesema muongozo huo ni njia itakayowawezesha wazalishaji wa mbegu na wakulima wa viazi kujiimarisha katika uzalishaji wenye tija kwa kujiendesha kibiashara zaidi.
“Muongozo huo unawaonyesha njia katika kada mbalimbali, kwanza namna bora ya usimamizi wa chama na vilevile mbinu bora za usimamizi wa fedha na mbinu bora za uendelezaji wa biashara.”Amesema Amon
Ameeleza muongozo utawaelekeza wazalishaji wa mbegu namna bora ya kufanya kazi pasipo kukiuka kanuni na sheria chini ya Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Nchini (TOSC).
Meneja wa CIP, Dk Kwame Ogero amesema mpaka sasa Tanzania inashika nafasi pili kwa uzalishaji wa viazi vitamu Afrika na iwapo kanuni za kilimo bora cha viazi zitafuatwa huenda ikapiga hatua kubwa zaidi.
Ofisa Utafiti kutoka TARI-Ukiriguru, Dk Hadija Mussa amesema muongozo utasaidia wazalishaji wa mbegu za viazi kutambulika zaidi na kupanua uwigo wa wafadhili wanaounga mkono zao hilo.