DAR ES SALAAM; Magwiji wa zamani wa timu ya Yanga wametembelea na kuipa mafunzo timu ya Safari Champion inayojiandaa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Yanga Juni 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Magwiji hao ni Edibily Lunyamila, Steven Nemes, Kenneth Mkapa, Said Maulid, Omar Hussein na Salvatory Edward.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Avic Town Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo timu hiyo imeweka kambi, Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Saad Kawemba amewataka vijana hao kuhakikisha wanapambana ili watimize malengo yao.
“Pambaneni mhakikishe mnatimiza malengo yenu kwa kufanya vizuri katika mchezo huo na kufuata yale mtakayofundishwa na wachezaji wa zamani, kwani michezo hujenga afya vile vile utawasaidia kupata ajira,” amesema Kawemba.
Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo ameipongeza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kutafuta vijana wenye vipaji kutoka mikoa mbalimbali na kufanikiwa kupata idadi ya wachezaji 22.
“Ninaipongeza TBL kupitia kinywaji cha Safari lager kuwakutanisha wachezaji wa zamani na vijana hawa, ikiwa pamoja na juhudi waliyoifanya kutafuta vijana wenye vipaji mikoa mbalimbali, ambao ninaamini miaka ijayo tutakuwa na wachezaji wazuri,” amesema Ndimbo.
Pia ameema wapo tayari kushirikiana na taasisi yoyote yenye nia ya kuendeleza soka la vijana hapa nchini kwa kuwa wanatambua michezo ina thamani kubwa.
Katika hatua nyingine Steven Nemes ambaye ni mlinda mlango wa zamani wa Yanga aliwataka vijana hao kufuata vizuri maelekezo wanayopewa na benchi lao la ufundi, kwani itawasaidia kufika mbali.