Mahakama Kuu Iringa yafungua mlango haki kwa wote

IRINGA: Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) kimesema mageuzi yaliyofanywa na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa katika miaka 20 ya uwepo wake yameleta mabadiliko makubwa katika namna wananchi wanavyofikiwa na huduma za haki.

Akiwa mwenyeji wa ugeni wa viongozi wa Mahakama Kuu chuoni hapo, Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo, Kaleb Lameck Gamaya (Adv), alisema mafanikio ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ni mfano unaoonyesha namna uwekezaji katika upatikanaji wa haki unavyoweza kubadili maisha ya watu wa kawaida.

“Kwa miaka 20 sasa, Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imekuwa nguzo muhimu. Imeleta haki karibu, imepunguza gharama, imeharakisha mashauri na imetupunguzia safari za mbali kutafuta haki. Haya si mambo madogo,” alisema Gamaya.

Ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wanafunzi wa sheria wa UoI sasa hupata mafunzo ya vitendo ndani ya mkoa huo kwa kutumia mashauri yanayosikilizwa katika mahakama hiyo—hatua ambayo imeongeza ujuzi kwa vitendo na kupunguza changamoto zilizowakumba wanafunzi kwa miaka mingi.

“Zamani tulikuwa tunategemea safari ndefu za mafunzo. Leo mashauri yapo hapa hapa. Wanafunzi wanajifunza vizuri zaidi, na wananchi nao wananufaika kwa kupata huduma kwa wakati,” amesema.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Gamaya ametoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwenye kliniki za sheria zinazoendeshwa na UoI kwa ushirikiano na wadau wa mahakama, akisema ni fursa ya kupata ushauri na msaada wa kisheria bure.

Amebainisha pia kuwa chuo hicho kupitia Kitengo cha Msaada wa Kisheria (Legal Aid Unit) kimekuwa kikihudumia idadi kubwa ya wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kisheria, ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, matunzo ya watoto, na mikataba ya ajira.

“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna anayenyimwa haki kwa sababu tu ya kukosa uwezo wa kumlipa mwanasheria,” alisema.

Maadhimisho ya miaka 20 ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa yanaendelea kwa kampeni za elimu kwa umma, ziara za kitaaluma na utoaji wa huduma za kisheria, yakilenga kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazochochea uwazi na upatikanaji wa haki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button