Mahakama yaamuru mmiliki hospitali kulipa mil 24.8

DAR ES SALAAM: MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuamuru mmiliki wa Hospitali ya Salamaan, Dk Abdi Warsame ,60, kulipa kiasi cha Sh milioni 24.8 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuisababishia hasara serikali wakati akiomba kibali cha makazi daraja C.
Mahakama hiyo imemuhukumu kulipa faini ya kiasi cha Sh milioni 2 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu na miezi minane gerezani baada ya kupatikana na hatia katika mashitaka mengine aliyokuwa akikabiliwa nayo.
Raia huyo wa Canada mwenye asili ya Somalia alikuwa akikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la kutoa tamko la uongo wakati wa kuomba uraia daraja C.
Hukumu hiyo imetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mushi amesema kuwa upande wa mashtaka umefanikiwa kuthibitisha hatia ya mshitakiwa pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo.
Kabla ya kusomwa kwa adhabu hiyo, Hakimu Mushi aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema na Wakili wa Serikili, Cathbert Mbilingi aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama yake.
Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Mushi amesema kuwa mshtakiwa katika kosa la kwanza na la pili anatakiwa kulipa faini ya Sh 25,000 kwa kila kosa au kwenda jela mwezi mmoja wakati shitaka la tatu, la nne na shitaka la tano mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh 500,000 kwenye kila kosa au kwenda jela miezi sita, huku kwenye shitaka la sita mshtakiwa Warsame ametakiwa kulipa faini ya Sh 500,000 au kwenda jela miezi sita.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imesema kuwa upande wa mashtaka umeibitisha pasipo kuacha shaka kuwa hasara aliyoisababisha mshtakiwa kiasi cha dola za marekani 10,000 na siyo Dola 12,500 kama ilivyo katika hati ya mashtaka, hivyo amemuamuru mshtakiwa kuilipa hasara hiyo kwa fedha za Tanzania ambazo ni sawa na Sh 24,865,000.
Pia ameamuru vibali vya mshtakiwa vya kufanya kazi visisitishwe kwani ni halali, mshtakiwa ni muwekeezaji na ameajiri watu wengi na pia inaonyesha mwaka 2023 alisajili vibali halali.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka matano ya kutoa matamko ya uongo wakati akiomba kibali cha ukaazi daraja C na shitaka moja la kuisababishia, Idara ya Uhamiaji hasara ya zaidi ya Dola 12,500.
Katika shitaka la kwanza ilidaiwa kuwa kati ya Julai 2014 na Oktoba 2014 katika ofisi za uhamiaji zilizopo Kurasini, wilayani Temeke Dar es salaam mshtakiwa akiwa si raia na ni muwekwezaji, alitoa tamko la uongo kwa Kamisha Mkuu wa uhamiaji wakati akiomba kibali cha makazi daraja C na kifanikiwa kupata kibali hicho kwa namba RPC1017007 huku akijua kwamba yeye ni muwekezji na mmiliki wa kampuni za Salaaman Health Service Limited na Salamaan Enterprises Ltd na hastahili kuwa na kibali cha makazi daraja C.
Pia mshtakiwa katika tarehe na miaka tofauti mwaka 2016, 2018, 2020 na 2021 alijipatia vibali kwa namba tofauti tofauti vya makazi wakati akijua yeye ni muwekezji na hastahili kupata vibali hivyo.
Katika shtaka la kuisababishia Serikali hasara, mshtakiwa anadaiwa kati ya Julai 2014 na Septemba 2021, Wilaya ya Temeke kwa makusudi alitoa tamko la uongo kwa Kamishna Mkuu wa uhamiaji wakati akiomba kibali cha makazi daraja c na kuisababishia uhamiaji hasara ya Dola 12,500.



