Mahakama yamuachia Dk Slaa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Balozi mstaafu, Dk Wilbroad Slaa (76) baada ya Mkurungenzi wa Mashtaka nchini (DDP) kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Dk Slaa anakabiliwa na mashitaka ya kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa X zamani ukifahamika kama twitter kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya kimtandao.
Aliachiwa huru mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Franco Kiswaga kesi hiyo ilipoletwa.
Hakimu Kiswaga alisema kesi hiyo ina pande mbili ambazo ni maombi yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri pamoja na kesi ya msingi.
Mawakili wa Serikali Waandamizi, Job Mrema akisaidiana na Clemence Kato walidai kuwa maombi yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri ya kupinga dhamana ya mshitakiwa yaondolewe.
“Tunaomba hili liingie kwenye kumbukumbu za Mahakama kuwa tunaomba kuondoa maombi tuliyowasilisha upande wa mashitaka la kupinga dhamana ya mshitakiwa Slaa,” alidai Mrema.
Wakili wa Utetezi, Hekima Mwasipu alidai hana pingamizi katika hilo.
Hakimu Kiswaga alikubaliana na ombi la jamhuri na kuondoa maombi hayo.
Aidha, Mrema alidai katika kesi ya msingi iliyokuwa ikimkabili Dk Slaa, Mkurungenzi wa Mashtaka nchini (DDP) hana nia ya kuendelea nayo.
“Tunaomba kutoa taarifa mbele ya mahakama yako kuwa upande wa Jamhuri chini ya kifungu cha 91 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 kwa niaba ya DPP kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya Dk Slaa kwa kosa ambalo ameshitakiwa nalo na linavyosomeka kwenye hati ya mashitaka,” alidai Mrema.
Hakimu Kiswaga alisema ombi hilo limekubaliwa chini ya kifungu kilichotajwa, hivyo Mahakama inamwachia huru mshitakiwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ilidaiwa kuwa Januari 9, 2025 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mtandao wa X wenye jina Maria Sarungi Tsehai, Dk Slaa alisambaza taarifa kwa nia ya kudanganya umma wa Watanzania huku akijua kuwa taarifa hiyo ni ya uongo.



