Mahakama Yaruhusu Uteuzi Mpya wa IEBC

NAIROBI: MAHAKAMA Kuu jijini Nairobi imeruhusu kuapishwa kwa Mwenyekiti mpya na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), baada ya kutupilia mbali ombi lililopinga uteuzi huo.
Jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Roselyne Aburili, wakishirikiana na majaji John Chigiti na Bahati Mwamuye, limesema kwamba ombi hilo, lililowasilishwa na Kelvin Ray Omondi pamoja na Boniface Mwangi, halikuzingatia misingi ya kisheria na halikuwasilishwa kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha Katiba.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, hakuna kizuizi tena kwa Erustus Ethekon Edung kuapishwa kama Mwenyekiti mpya wa IEBC, sambamba na makamishna Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol na Fahima Araphat Abdallah.
Hata hivyo, mahakama imefuta tangazo la awali la gazeti la serikali lililotolewa na Rais William Ruto kuhusu uteuzi huo, ikielekeza kutolewa kwa tangazo jipya ili kuhalalisha mchakato huo kikatiba.



