SENSA ya Watu na Makazi nchini iliyofanyika Agosti 23, mwaka 2022, imefanyika kwa mafanikio makubwa na watu asilimia 99.99 wameitikia kuhesabiwa katika maeneo yao.
Sensa ya watu na makazi, inafanyika kila baada ya miaka 10 na mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2012. Tofauti na sensa zilizopita Sensa ya mwaka 2022, ni kwanza ya kidijiti na ishirikisha mambo matatu pamoja, sensa ya anuani za makazi, majengo na watu na makazi.
Kamisaa wa Sensa ya Sita Tanzania Bara ambaye ni Spika mstaafu, Anne Makinda anasema anajivunia kutekeleza kikamilifu wajibu wake wa kuhamasisha umma wa Tanzania kujitokeza kuhesabika na hatimaye kupata takwimu bora za aina mbalimbali tangu kwenye mitaa na vitongoji.
“Najivunia kufanikiwa kwa sensa hiyo ambayo imetokana na uhamasishaji mkubwa uliofanyika hadi katika ngazi za vitongoji,” anasema.
Licha ya baadhi ya maeneo kuwa na mazingira magumu kufikika, makarani walifika na uthibitisho unaonesha wazi kutokana na takwimu zilizopatikana ambazo zinaonesha kila kitu kilichopo.
Kutokana na hamasa kubwa kufanyika kwa kutembelea wananchi hata mara tano katika maeneo mbalimbali, hata maeneo ambayo katika sensa ya 2012 watu waligoma kuhesabiwa katika sensa ya mwaka 2022, kila mtu aliyelala nchini usiku wa kuamikia Agosti 23 alihesabiwa.
Makinda akizungumza na waandishi wa magazeti ya Serikali ya HabariLEO, Dailynews na Dailynews Digital hivi karibuni anasema, tangu mwaka jana baada ya kukamilika sensa, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imekuwa na kazi ya kuchakata taarifa na takwimu hizo na kupeleka mrejesho kwa wananchi kwa kuwaonesha kila kitu kinachopatikana katika maeneo yao.
Makinda (73) anasema, Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, imesaidia kuleta mageuzi makubwa ya takwimu nchini. Kwa kufanyika Sensa ya kidijiti, Tanzania imeandika historia nchini na nje ya nchi na sasa takwimu bora zinapatikana.
“Takwimu zimepatikana, hivyo wajibu wa viongozi na wananchi katika ngazi hadi kwenye vitongoji kuzitumia takwimu katika kujiletea maendeleo,” anasema.
Takwimu hizo ambazo zinatakiwa kutumika kitaifa na kimataifa, zimelifanya taifa na wananchi wake kujua idadi ya watu, shughuli zao za maendeleo na miundombinu iliyopo.
Makinda anasema matokeo ya sensa yamefungua ukurasa mpya wa takwimu nchini kwani hivi sasa taasisi za kimataifa badala ya kuja kutafuta takwimu nchini kabla ya kuamua kuwekeza au kutoa huduma zinapata takwimu zikiwa katika nchi zao.
Mashirika ya kimataifa yanajua takwimu za Tanzania huko huko yalipo na hivyo ni rahisi kwao kuamua kuja kuwekeza au kutoa huduma nchini katika maeneo yenye shida, uhitaji au yenye upungufu wa huduma fulani.
Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kutaka kuhesabiwa na hata kupiga simu ofisi za NBS kuomba kuhesabiwa, takwimu bora zimepatikana kutokana na Watanzania asilimia 99.9 kujitokeza.
Anasema takwimu hizo pamoja na mambo mengine zimeonesha nguvukazi ya vijana waliopo nchini ambao wanafikia asilimia 53.7. Hao ni vijana wanaoweza kufanya kazi na ndio rasilimaliwatu kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali za uzalishaji iwe katika ajira rasmi au ajira isiyo rasmi.
Makinda anasema: “Hakuna taifa lolote duniani ambalo linaweza kuajiri nguvu kazi zote ambazo zinazalishwa kwa kuhitimu kila mwaka kutoka kwenye vyuo mbalimbali”.
Kutokana na takwimu hizo ambazo zinaonesha ongezeko la wahitimu nchini, vijana wenyewe wanatakiwa kujiajiri kwa kufanya shughuli mbalimbali katika maeneo yao kutokana na serikali kuboresha miundombinu kama umeme, barabara, maji na huduma za afya.
“Serikali imerahisisha mawasiliano, kwa sasa hata vijijini wanaweza kufanya shughuli mbalimbali za kujiajiri kutokana na kuwepo kwa umeme na miundombinu ya barabara katika maeneo yao,” anasema.
Anasema uwepo wa miundombinu hiyo, utasaidia vijana wengi wanohitimu kozi mbalimbali na katika ngazi mbalimbali kuanzisha kazi au shughuli za ujasiriamali katika maeneo yao.
Makinda anasema wakati umefika kwa vijana na wananchi kwa ujumla kuachana na mtazamo wa kudhani kwamba ajira zinatoka serikalini. Mtazamo huo umepitwa na wakati kutokana na wahitimu kuwa wengi na ajira kuwa chache.
Anasema kwa wananchi uwepo wa takwimu zinazoonesha miundombinu mbalimbali wanaweza kuanza kujiandaa, mfano kujenga maboma ya zahanati na vituo vya afya, huduma za maji na huduma nyingine kulingana na idadi yao.
Takwimu hizo zimebainisha wazi baadhi ya huduma hazipatikana katika maeneo mengine ambako kuna idadi kubwa ya watu na mahali pengine ipo wakati idadi ya watu ni ndogo.
Lakini pia takwimu zimeonesha kwamba katika baadhi ya maeneo kuna uharibifu wa mazingira, kuna changamoto kubwa ya mazingira kuharibika. Katika maeneo hayo kampeni za kuboresha mazingira ikiwemo kupanda miti zinatakiwa kupewa msukumo.
“Katika baadhi ya maeneo hayana shule, basi wananchi wanaweza kuanza kuweka mkakati wa kujenga shule au zahanati katika maeneo yao, kwani hawana huduma hizo,” anasema.
Takwimu zimeonasha wazi kwamba kama jumla ya Watanzania ni milioni 61.7 anasema ni wazi kwamba idadi yao wananchi katika kitongoji, kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa wanajulikana vizuri idadi yao kwa jinsi, umri, wazee, watoto, vijana, wanawake na wanaume wa kila umri na aina nyingine.
Makinda anasema takwimu zilizopatikana ziwe chachu kwa serikali katika kuleta maendeleo sawia kwa maeneo yote na kwa wananchi wa maeneo husika wanatakiwa kuunga mkono serikali katika kujenga miundombinu ya maeneo yao.