MWANASIASA mkongwe nchini, Pius Msekwa (88) amesema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Serikali ya Wakoloni wa Kiingereza walikubaliana kuipatia Tanganyika uhuru Desemba 20, 1961 na si Desemba 9 ya mwaka huo.
Msekwa amesema mabadiliko hayo yalitokana na sababu za kiimani za utawala wa Uingereza chini ya Malkia.
Amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) nyumbani kwake Ukerewe mkoani Mwanza.
Msekwa akasema Nyerere aliyafurahia mabadiliko hayo na baada ya uhuru katika mfumo wa Katiba ya Uingereza, Malkia wa Uingereza aliendelea kuwa mkuu wa nchi ya Tanganyika huru.
Kwa mujibu wa Msekwa, Mwalimu Nyerere hakuibishia katiba hiyo kwa kuwa ulifanyika mkutano wa kikatiba Dar es Salaam na Waingereza walishiriki.
Anasema Nyerere na ujumbe wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) walishiriki kukubaliana kuhusu katiba hiyo.
“Mwalimu hakuibishia sana, alisema si kazi ya Waingereza kututungia sisi katiba, acha waondoke halafu tutatunga ya kwetu wenyewe.
“Alisema Waingereza wanashughuli gani na katiba ya nchi hii, alisema tuwakubalie waondoke, tutatengeneza katiba yetu wenyewe, ndivyo ilivyokuwa,” anasema Msekwa.
Anasema alichotaka Mwalimu si katiba bali ni tarehe ya uhuru kwamba lini uhuru utapatikana kwa kuwa tayari alishawaahidi wana TANU na Watanganyika kuwa uhuru ungepatikana kabla ya mwisho wa mwaka 1961.
Msekwa anasema kwa kuwa tarehe ya kwanza iliyokubaliwa ya kupata uhuru ni Desemba 20, Nyerere aliridhika na kufurahi na ndipo likatengenezwa bango lililosomeka ‘Complete Independence 1961.’
“Mwalimu Nyerere akafurahi, akalibeba lile bango na kutoka ndani ya mkutano huo kwa sababu lilikuwa limeshaandaliwa, akaingia kwenye gari na kufanya maandamano Dar es Salaam akionesha bango lile ‘Complete Independence 1961’,” anasema.
Msekwa anasema baada ya ujumbe wa Uingereza kurudi nchini mwao na kuripoti kwenye serikali yao, Malkia aliamua kuwa atakayetoa hati za uhuru ni mume wake mwenyewe, yaani angemtuma mumewe aje Tanganyika kutoa hati ya uhuru.
Anasema kutokana na mila zao za kifalme, Desemba 20 inaangukia katika wiki ya Krismasi na kwa ufalme wa Uingereza ndiye Mkuu wa dini ya Uingereza, Malkia akaona isingekuwa vema abaki peke yake katika wiki hiyo.
Msekwa anasema Malkia aliikataa tarehe hiyo ya Desemba 20 kutoa uhuru kwa Tanganyika kwa kuwa haikuwafaa wao kama watawala, hivyo wakaibadilisha tarehe hiyo kurudi nyuma hadi Desemba 9, 1961.
Baada ya kubadilisha tarehe hiyo, anasema Waingereza walimuuliza Nyerere kama Desemba 9 inamfaa au la, na ndipo Mwalimu akawajibu: “Ilimradi ni mwaka 1961 na tena ikiwa mapema zaidi itanipa raha zaidi kuwaeleza Watanganyika, kwa hiyo nakubali.
”
Baada ya uhuru
Msekwa anasema Januari mwaka 1962, Mwalimu Nyerere aliitisha mkutano wa chama cha TANU ili kuanza mchakato wa katiba anayoitaka na aliomba idhini ya chama kuanza mchakato wa kuandaa katiba mpya ya Tanganyika.
Anasema baada ya hapo, Mwalimu alijiuzulu Uwaziri Mkuu na kumwachia Rashid Kawawa na Mkuu wa nchi alikuwa bado Malkia wa Uingereza aliyekuwa anawakilishwa na Gavana Jenerali.
Msekwa anasema sheria zote zilizopitishwa wakati huo zilipelekwa kwa Gavana ili azikubali kwa niaba ya Malkia kwa kuwa sheria za nchi huwa zinakubaliwa na mkuu wa nchi tangu wakati huo mpaka sasa.
Anasema mchakato huo wa kupata katiba mpya ya Tanganyika huru ulianza Januari 1962 na ulichukua mwaka mzima na uamuzi wa kutaka Tanganyika iwe Jamhuri ulifanyika ili wasiendelee na utaratibu wa Malkia kuwa mkuu wa nchi.
Msekwa anasema nchi inapokuwa Jamhuri maana yake Mkuu wa nchi au Rais anatokana na kuchaguliwa na wananchi wenyewe, hivyo wakaamua kujiondoa kwa Waingereza na kuanza kujitegemea.
Anasema katiba hiyo ilifanyiwa kazi na ilipofika Novemba 1962 mchakato ukakamilika na sheria za uchaguzi wa rais zikawa zimeshapitishwa na Bunge.
“Kwenye Novemba hiyo hiyo ukafanyika uchaguzi wa Rais na wakagombea watu wawili, Mwalimu Nyerere na Zuberi Mtemvu. Wakati ule Mtemvu alikuwa kiongozi wa Chama cha African National Congress (ANC), alijitoa kutoka TANU kwa kuwa alitofautiana na TANU kwa sababu alitaka nchi iwe ya Waafrika tu hakutaka tena wahindi na wazungu wapate uraia, alitaka Tanganyika huru yenye Waafrika tu,” anasema Msekwa.
Anasema Mwalimu Nyerere alipata ushindi kuwa Rais na aliapishwa Desemba 9, 1962 yaani mwaka mmoja baada ya uhuru au siku waliyotimiza mwaka mmoja wa uhuru kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika chini ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Tanganyika.
Uteuzi
Msekwa anasema siku hiyo ya Desemba 9, 1962 ilikuwa siku ya bahati njema kwake kwa kuwa baada ya Mwalimu Nyerere kuapishwa kuwa Rais, akamteua yeye kuwa Katibu wa Bunge.
Anasema wakati huo Waingereza walishatoka kwenye nafasi hizo kwa kuwa zilipitishwa sheria zinazotaka asiyekuwa raia wa nchi kutokuwa kiongozi wa serikali, hivyo Katiba ya Jamhuri ikawaondoa akiwamo Spika wa Bunge aliyekuwa Mhindi akiitwa Karimjee aliyekuwa na uraia wa Uingereza na hakutaka kuubadilisha.
Msekwa anasema sheria ikamfuta Spika huyo na Adam Sapi akachaguliwa kuwa Spika wa kwanza Mtanzania na Katibu wa Bunge aliyekuwa Mwingereza naye sheria ikamfuta na kuteuliwa yeye kuwa Katibu wa Bunge.
Anasema uteuzi huo wa kuwa Katibu wa Bunge ulimfanya kuingia hatua mpya ya uhusiano na Mwalimu Nyerere kwa kuwa sheria zinapopitishwa na Bunge hupelekwa kwa Mkuu wa nchi kwa ajili ya kuidhinishwa, yaani kuwekewa saini ya kukubali ambapo kwa Kiswahili inaitwa ‘Nakubali’ kisha anasaini juu ya maneno hayo kwa mfano JK Nyerere.
Kwa kuwa kazi mojawapo ya kikatiba ya Rais baada ya kuchaguliwa ni kulifungua Bunge, anasema Desemba 10, yaani siku moja baada ya kuapishwa kuwa Rais, Mwalimu Nyerere alilifungua Bunge chini ya Spika Sapi na Katibu mpya wa Bunge Msekwa.
“Sasa nikaanza utaratibu mpya, badala ya mesenja kupeleka muswada Ofisi za Ikulu kwa utaratibu wa kawaida, nikasema nitapeleka mwenyewe. Nikaleta ubunifu wangu wa kuipeleka mwenyewe Ikulu,” anasema Msekwa.
Sheria kufuta machifu
Anasema wakati huo baada ya uhuru kulikuwa na sheria ya kufuta machifu, hivyo alipoipeleka miswada iliyopitishwa na Bunge ukiwamo huo wa machifu, Mwalimu Nyerere alimuuliza hali ilikuwaje ndani ya Bunge ili kujua tu kama kulikuwa na upinzani wowote.
“Nikamwambia hakukuwa na upinzani Mheshimiwa, wote waliochangia waliunga mkono pamoja na Chifu Fundikira mwenyewe aliunga mkono kwa niaba ya machifu wenzake, Chifu Fundikira alikuwa Mbunge, hivyo hata yeye aliunga mkono, ooh, nikamfurahisha,” anasema Msekwa.
Anaongeza: “Basi tukapigapiga soga nyingine kidogo hapo, nikaona anaupenda huo utaratibu, kuanzia hapo kila muswada unaopitishwa mimi nikawa nampelekea mwenyewe ofisini kwake, basi tukajenga mahusiano ya karibu sana.”
Sababu kufuta machifu
Msekwa anasema Mwalimu Nyerere alizieleza mwenyewe sababu za kufuta machifu ikiwamo kutaka kujenga utaifa au taifa moja kwa kuwa machifu walikuwa wa kabila moja moja na utii wa watu ulikuwa kwa machifu wao, hivyo asingeweza kujenga umoja wa nchi baada ya uhuru.
“Ili kuleta utii kwa taifa moja, ilibidi kufuta huo utii mdogo mdogo kwa machifu ili isiwe kikwazo kwa kujenga utii mmoja kwa kiongozi mmoja wa Taifa moja, hii hasa ndio ilikuwa sababu kubwa katika juhudi za kujenga utaifa wa Taifa la Tanganyika, vinginevyo kila kabila lingeendelea na chifu wao ingekuwa vigumu kuunda taifa moja linaloweka makabila yote pamoja,” anasema Msekwa.
Anaongeza: “Ndiyo maana nilipoupeleka ule muswada aliuliza hali ilikuwaje ndani ya bunge, alitaka kujua kama hoja zake zilitosha na zilikubalika au kulikuwa bado na upinzani. Nikamwambia Mzee hapakuwa na upinzani wowote, ilikuwa kujenga utaifa na uzalendo mmoja na utiifu kwa taifa.
”
Anasema aliendelea kuwa Katibu wa Bunge kwa takribani miaka 10 mfululizo mpaka mwaka 1970, hivyo hata Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulimkuta akiwa Katibu wa Bunge.