MWANZA – WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofi si ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Ofi si ya Waziri Mkuu zikae na Wizara ya Fedha na kuandaa mpango wa kitaifa kuwawezesha vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya wajikimu.
Majaliwa alitoa agizo hilo jijini Mwanza jana wakati akizungumza na wananchi na wadau walioshiriki kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani.
“Wako wengine wanaohitaji kilimo, wizara ya kilimo itoe utaratibu, wapo wanaohitaji ufundi, wizara ya elimu itoe utaratibu, lengo ni kuhakikisha vijana hawa wakitoka huko wanakuwa na shughuli ya kufanya ili kujikimu,”alisema.
Aliongeza: “Kamishna Jenerali pamoja na timu yako ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya endeleeni kufanya operesheni dhidi ya dawa za kulevya kwenye mabasi, ndege, bandarini, vituo vya reli, masoko, maeneo yenye watu wengi, kote nchini ili kuhakikisha kuwa tunaendelea kubaki salama”.
MWANZA – WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu zikae pamoja na Wizara ya Fedha na kuandaa mpango wa kitaifa wa kuwawezesha kujikimu vijana wanaoachana na matumizi ya dawa za kulevya nchini. pic.twitter.com/PufVVR8cH0
— HabariLeo (@HabariLeo) June 30, 2024
Majaliwa alihimiza wananchi wote wakiwemo wazazi, walezi, viongozi wa dini na taasisi za afya waendelee kupiga vita dawa za kulevya kwa vitendo.
“Sote tuna wajibu wa kuwafundisha watoto wetu namna bora ya kuishi kwa kufuata maadili na kujiepusha na tabia na makundi rika yanayoweza kuwashawishi kuingia kwenye janga la matumizi na biashara ya dawa za kulevya,” alisema.
Katika tukio hilo Majaliwa alizindua Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2024. “Napenda kuwahimiza sote tujitolee kikamilifu kutekeleza Sera hii ya Taifa. Tuwe walinzi wa vijana wetu na tukishirikiana, tunaweza kufanikisha lengo la kuwa na jamii salama na yenye afya njema,”alisema.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana), Jenista Mhagama alisema sera hiyo itakuwa na matamko yatayokwenda kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Jenista alisema sera hiyo itasisitiza utoaji wa elimu kwa waraibu wa dawa za kulevya, elimu kwa watumiaji wote wa dawa ili serikali iweze kufanya udhibiti wa kutosha kwenye matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Alisema pia sera hiyo inahusu utaratibu wa utoaji wa kinga, matunzo na matibabu kwa Waraibu ambapo alikiri eneo hilo bado halijafanyiwa kazi vya kutosha.
SOMA: Treni ya Haraka kuanza safari za Dar – Moro
“Sera yetu pia inalenga kuboresha udhibiti wa mimea inayozalisha dawa za kulevya, ikiwemo bangi na mirungi na tumeishaanza kufanya kazi na Wizara ya Kilimo kuona ni namna gani tutafanya kazi kwa pamoja kwenye udhibiti, ”alisema Jenista.
Alisema Rais Samia amefanya uwekezaji kwenye maabara ya taifa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali kwa kununua mashine ya kisasa iliyopewa ithibati na Umoja wa Mataifa inayoshughulikia mapambano dhidi ya dawa za kulevya Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA), Aretas Lyimo alisema katika kipindi cha Juni, 2023 hadi Mei 2024, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine walikamata zaidi ya kilo milioni mbili za dawa ya kulevya kiasi ambacho ni kikubwa kukamatwa katika kipindi cha miaka 11.